Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu ch Sayansi na Teknolojia (Must), Profesa
Joseph Msambichaka (mwenye miwani katikati) akifuatilia maelezo ya
wanafunzi kuhusu utengenezaji wa roboti. Picha na Lauden Mwambona
Wakati vijana wengi wanaomaliza vyuo mbalimbali wakikosa kazi,
wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (Must) cha
jijini Mbeya kwa kushirikiana na serikali ya Italia, wanatarajia kutoa
mafunzo kwa vijana kuhusu utengenezaji wa roboti zinazosaidia kufanya
kazi viwandani.
Mafunzo hayo yataanza Oktoba mwaka huu na
yatalenga kutengeneza roboti zitakazofanya kazi kwenye viwanda
mbalimbali vikiwamo vya kutengeneza sukari, nguo, dawa, sabuni na
bidhaa nyingine mbalimbali.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Joseph
Msambichaka anasema mpango huo wa mafunzo kwa ngazi ya stashahada
unatekelezwa kwa ushirikiano na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha
Polytechnic of Milan cha Italia.
Anasema wameanza kwa kuwafundisha wahadhiri 12
kutoka vyuo vitatu nchini, ambao wamefanikiwa kufaulu na kutengeneza
roboti moja linaloweza kufanya kazi kwenye kiwanda.
‘’Kazi za kisayansi na teknolojia hazihitaji mtu
kushika nyundo ili kuzitekeleza, bali zinahitaji utalaamu wa kisasa
ukiwamo wa kutumia roboti ili kurahisisha utendaji’’ anasema Profesa
Msambichaka.
Meneja wa mpango huo kwa upande wa Italia kupitia
Ubalozi wake uliopo Dar es Salaam, Daniele Cristian Passalacqua
anasema Serikali yake iliamua kuisaidia Tanzania katika masuala ya
teknolojia ya matumizi ya roboti kwa lengo la kuongeza kasi ya
maendeleo nchini.
Anasema Italia kupitia Chuo Kikuu cha Milan
itashirikiana na Tanzania kuhakikisha teknolojia hiyo inakuzwa na
kufanyiwa kazi kwa lengo la kurahisha kazi na kuongeza ufanisi.
‘’Tayari Serikali yangu inasaidia elimu ya
sayansi kwa wasichana wanaosoma vyuo mbalimbali na hadi sasa wapo
wasichana 500 wanaosomeshwa kupitia mpango huu’’ anasema Cristian.
Anasema mpango wa kufundisha masomo ya
kutengeneza roboti utatekelezwa kwenye vyuo vya Sayansi na Teknolojia
Mbeya, Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Ufundi
Arusha.
Ofisa huyo anasema matumizi ya roboti katika
masuala ya sayansi na teknolojia nchini, yataiondoa Tanzania kwenye
kundi la nchi Masikini zaidi duniani na kuifanya iwe nchi yenye
maendeleo.
Naye Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha
Polytechnic Of Milan, Profesa Francesco Braghin ambaye alifika kutoa
mafunzo kwa wahadhiri watakaofundisha utengenezaji wa roboti nchini,
anasema dunia ya tatu inahitaji roboti ili kuboresha kazi.
Anasema wanaamini kazi zikifanywa kwa roboti
zitafikiwa malengo na uzalishaji utaongezeka kwa vile roboti haina
kupoteza muda wala kufanya uzembe ili mradi uipange vizuri.
Mratibu wa mpango huo katika Chuo Kikuu ch Sayansi na Teknolojia
Mbeya, Dk Lusajo Muga anasema chuo chake kimeupokea kwa moyo mkunjufu
mpango huo, baada ya kubaini ukweli kwamba dunia ya leo siyo ya jana.
Muga ambaye ni mwanamke bingwa katika kitivo cha
Uhandisi wa Kompyuta anasema Italia imewasaidia kupata vifaa mbalimbali
va maabara na kwamba malengo ni kuwasomesha wasichana wengi zaidi
kutokana na ufadhili kwao unaotolewa na nchi hiyo.
Anasema Italia imewafadhili wasichana mbalimbali
wanaosomea masuala ya sayansi na teknolojia katika chuo chake , hivyo
anawahimiza wasichana kuongeza bidii ili waweze kufaidi matunda ya
msaada huo.
Anna Kisoki kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es
Salaam ambaye ni mmoja wa watakaofundisha roboti nchini, anasema ana
uhakika kwamba wanafunzi watayapenda zaidi masomo hayo kwa vile
yatashirikisha zaidi vitendo.
Anasema wanafunzi watajifunza kutengeneza roboti
na kuitumia katika kazi za kila siku, jambo ambalo anaamini litaongeza
uzalishaji na ufanisi wa kazi.
‘’Roboti zikitumika kupanga chupa za vinywaji
viwandani ama kupanga viroba vya sukari na hata kujaza dawa kwenye
chupa, kazi itafanyika kwa urahisi na haraka zaidi’’ anasema Kisoki
akieleza faida za matumizi ya roboti maeneo ya kazi.
Post a Comment