0
Wengi hujikuta wakipigwa, wakitukanwa, wakinyanyaswa au wakipewa adhabu kali na walimu wao kutokana na hali zao wakiwa darasani.
Ni maisha ya kawaida tu kwao, japo si hiyari yao hayo yatokee. Mambo wanayotendewa wanafunzi hawa yamekuwa sugu kiasi cha kuwafanya wasisome kwa umakini na hatimaye kutengwa na mfumo mzima wa elimu stahiki.
Hawa ni  wanafunzi wenye mahitaji maalumu, wakiwamo walemavu wanaojulikana zaidi katika jamii.
Kimsingi wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni kundi la watoto mbalimbali nchini wakiwamo wale wanatoka kwenye familia duni, waliotelekezwa, wenye ulemavu wa aina zote, wenye matatizo ya kisaikolojia na wengineo.
Kundi hili kwa bahati mbaya limejikuta likitengwa na jamii husika kwa kuwa walimu na wazazi hawajabaini haraka mahitaji yao ambayo yamekuwa ya nadra sana kusikika au kubainika.
Suala hili ndilo lililowakutanisha wadau mbalimbali wa elimu  hivi karibuni kujadili namna kundi hilo litakavyosaidiwa ili lipate elimu bora.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), wadau wanabainisha kuwa watoto wengi wamekuwa wakihudhuria darasani na kutoka bila ya kuelewa chochote kutokana kukosa msaada madhubuti kutoka kwa walimu wao.
Hali hii kwa mujibu wa wadau hao inaendelea mpaka wanapohitimu na kupata alama mbaya na hatimaye kutupwa nje ya jumuiya ya wasomi.
Uelewa mdogo
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam, Dk Luka Mkonongwa anasema utamaduni wa kutobaini mahitaji maalumu ya wanafunzi katika ngazi za chini ndiyo uliofanya watoto wengi nchini kutengwa.
Elimu jumuishi ni ile inayozingatia mahitaji ya watoto wote kwa kutoa elimu bora kwa usawa bila kuangalia vigezo vya uwezo wa kiakili, afya, ulemavu na fedha, anasema na kuongeza:
“Utakuta mwalimu anamwadhibu mwanafunzi anayesinzia darasani au anampigisha magoti yule ambaye haelewi darasani bila kufahamu  kuwa yule mtoto ana matatizo gani yanayomsumbua. Hilo ni tatizo la kulitatua haraka.’’
Anasema: “Walimu wengi hawana uelewa juu ya elimu jumuishi. Hawajafunzwa kabisa, hivyo ni vigumu kuwajali watoto wa aina hii kwa kuwafundisha katika mazingira rafiki.”
Hoja ya Dk Mkonongwa inaibua mjadala mzito ambao unang’amua kuwa hata kwenye vyuo vya ualimu elimu jumuishi haifundishwi ipasavyo na ni taasisi chache zinazotoa kozi zinazofanana na elimu hiyo.
“Ni vyuo vikuu vinne vinavyotoa kozi za elimu maalumu ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Sebastian Kulowa, Lushoto.
“Hivi vina kozi moja moja tu inayoweza kusaidia kujenga msingi wa elimu jumuishi wakati Chuo cha Patandi  cha Arusha ndicho pekee kinachofundisha walimu ufundishaji wa watu wenye mahitaji maalumu,” anasema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Mkwawa, Daniel Hyera.
Hyera anabainisha uchache wa vyuo hivyo unaweka wazi kuwa ni vigumu walimu kufahamu vizuri namna ya kuwalea na kuwafundisha watoto wenye matatizo mbalimbali.
Pia, wazazi nao hawajafahamishwa aina hii ya elimu kutokana na kukosa fursa ya kupatiwa mafunzo.
Mwalimu Raphael Njiwa wa shule ya sekondari Kaseme iliyopo mkoani Geita, kwa upande wake anakiri kuwa ni walimu wachache wanaojitoa kuwasikiliza watoto na kuwafundisha kulingana na mahitaji yao.
“Kuna wakati unaguswa unamsikiliza mwanafunzi baada ya kugundua nidhamu au ufanisi wake darasani umeshuka. Wale wanaokueleza unawapa ushauri na kuwasaidia waweze kuelewa kama wengine,” anasema Njiwa.
Sera na mitalaa ni tatizo
Hata hivyo, si lawama kwa vyuo pekee kushindwa kufundisha walimu kuelewa mahitaji maalumu ya wanafunzi, bali hali hiyo inaikumba pia serikali kwa kushindwa kuandaa mazingira rafiki ya kuwezesha jitihada hizo.
Serikali inalalamikiwa kushindwa kuandaa sera na mikakati madhubuti ya kutekeleza elimu jumuishi katika ngazi zote.
Pia, utekelezaji wa kususua kwa baadhi ya sera na mitalaa rafiki kwa elimu bora na inayoleta usawa, unatajwa kuwa chanzo cha kuwakosesha baadhi ya Watanzania elimu bora.
“Mitalaa mingi imelenga tu katika maudhui badala ya kufanikisha uweledi na uelewa wa mwanafunzi. Hali hii inawajenga watoto kukariri tu masomo badala ya kuelewa kinachozungumziwa na hatimaye kuwatenga wengine,” anasema mtaalamu wa masuala ya elimu, Dk Wilberforce Meena.
Anasema kuwa serikali ina sera nzuri za kuvutia lakini utekelezaji wake siyo wa kuridhisha kiasi cha kutishia mustakabali wa elimu.

Post a Comment

 
Top