Wiki moja iliyopita, timu ya taifa ya soka, Taifa Stars ilicheza
mechi ya kwanza ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza Fainali za
Mataifa ya Afrika (CAN 2015) dhidi ya Msumbiji na kutoka sare ya 2-2
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Fainali hizo za 30 za Mataifa ya Afrika
zinatarajiwa kufanyika nchini Morocco kuanzia Januari 17 mpaka Februari
8, 2015 na zitashirikisha timu 16.
Mwishoni mwa wiki hii, Taifa Stars itaingia tena
uwanjani kucheza mechi ya marudiano na wapinzani hao kwenye Uwanja wa
Zimpeto mjini Maputo kuwania kutinga hatua ya makundi kabla ya kupata
timu mbili zitakazofuzu kucheza fainali hizo nchini Morocco.
Kama Taifa Stars itaibuka na ushindi katika mechi hiyo, itaingia Kundi F lenye timu za Zambia, Cape Verde na Niger.
Ni wazi baada ya Taifa Stars kutoka sare ya mabao
2-2 na Msumbiji wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam imejiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele.
Hata hivyo, huu siyo wakati wa wachezaji wa Stars,
viongozi wa soka, Serikali na mashabiki nchini kukata tamaa kwa sababu
ipo mechi ya marudiano mwishoni mwa wiki hii ambayo tunatakiwa kuitumia
vema kupata ushindi ingawa tutakuwa ugenini.
Tunaamini vijana wa Taifa Stars hawatakata tamaa
ila watacheza kwa uwezo wao wote kuhakikisha wanapata matokeo
yatakayoiwezesha timu kuvuka hatua hiyo muhimu katika safari hiyo ya
kuelekea Morocco.
Tunatarajia wachezaji wa Stars watalipigania taifa
kwa hali na mali, kuweka ubinafsi kando na kuwa kitu kimoja kuhakikisha
wanapata matokeo yanayotakiwa ili timu isonge mbele.
Katikia mchezo wa kwanza tuliona udhaifu wa
wachezaji kupoteza umakini uwanjani na hivyo kuigharimu Taifa Stars.
Wachezaji wanatakiwa kufahamu wajibu walionao katika timu ya taifa.
Tunasema hivyo kwa sababu tunafahamu kazi ya
mchezaji wa timu ya taifa ni kupigania kitu ambacho huwa na thamani na
kumbukumbu kubwa kwa vizazi vingi vitakavyofuatia.
Kitu wanachotakiwa kuleta wachezaji wa timu ya
taifa ni ushindi. Siku zote wachezaji wa timu ya taifa wanaposhinda huwa
wanaliletea taifa lao furaha na kujisikia fahari kuishi katika taifa
hilo, hivyo tunatarajia wachezaji wa Taifa Stars wanaelewa wana jukumu
kubwa la kutuletea furaha wananchi wa Tanzania na kutengeneza historia
zao kwa kuanzia mechi hii ya marudiano dhidi ya Msumbiji.
Tunatarajia uongozi wa timu pamoja na uongozi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) wanakuwa karibu na wachezaji ili
kuwatia nguvu na kuwapa kile ambacho kitaonekana ni muhimu kwa mchezo
huo.
Itakuwa ajabu basi kusikia lawama zikitupiwa kwa watu tofauti
kama timu itafanya vibaya, hiyo itamaanisha mtu fulani hakutimiza wajibu
wake fulani kwenye timu na hivyo kusababisha matokeo mabaya.
Tunatarajia kutosikia hayo na badala yake kusikia
lugha moja hata kama matokeo hayatakuwa mazuri au pale tutakapopata
matokeo mazuri.
Vilevile tunatarajia kuona TFF, wadhamini,
mashabiki pamoja na serikali wakiendelea kumpa ushirikiano mzuri kocha
Mart Noiij ili aweze kuwandaa vizuri wachezaji wa Taifa Stars ili
kuhakikisha ushindi unapatikana katika mechi ya marudiano dhidi ya
Msumbiji.
Tunaelewa Taifa Stars ina kibarua kigumu, lakini
pia tunaamini tuna wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa kuliko
wachezaji wa Msumbiji hivyo hatutakiwi kukata tamaa ya ushindi mwishoni
mwa wiki.
Post a Comment