0
Dar es Salaam. Tatizo la hitilafu ya umeme limeonekana kuwa chanzo kikubwa cha ajali nyingi za moto zinazotokea wilayani Kinondoni jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa mali na kurudisha nyuma maendeleo.
Jana moto uliteketeza maduka sita yaliyopo katika Mtaa wa Mnazini Mwananyamala, jijini Dar es Salaam. Moto huo uliteketeza maduka ya vifaa vya ushonaji, makabati, majokofu na ofisi moja ya fundi cherehani.
Diwani wa Kata ya Makumbusho, Haroub Ally alisema tukio hilo ni la nne kutokea katika kata yake na matukio yote yanadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme. Alisema kuna haja kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kurekebisha mifumo ya zamani ili kuzuia majanga hayo.
Ally alilalamikia pia uchache wa magari ya zimamoto na kushauri kuwa imefika wakati sasa kwa kila wilaya iwe na magari hayo ili iwe rahisi kufika katika maeneo ya ajali kwa wakati. Alisema kwa sasa kuna kituo kimoja tu kinachotegemewa na maeneo mengi, hali inayowafanya washindwe kutoa huduma hiyo kwa wakati.
“Moto ulianza tangu saa tano asubuhi na tukatoa taarifa kwa Kikosi cha Zimamoto, lakini wamefika hapa saa saba. Chakushangaza wamefika na gari ambalo halina maji, sasa sijui walikuja kufanya nini,” alihoji diwani huyo.
Naye mmiliki wa duka la vifaa vya ushonaji, Hassan Kamadu alisema alihamia katika nyumba hiyo miezi miwili iliyopita na hakuwahi kuona tatizo lolote la umeme. Alisema moto huo umeteketeza mali zake zenye thamani ya Sh50 milioni.
Kamadu ambaye hakuwa na bima ya biashara wala ya moto, alisema hana la kufanya kwa sasa. na yote amemuachia Mungu.

Post a Comment

 
Top