Morogoro. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa
ya Morogoro, Dk Ritha Lyamuya amesema hali ya mtoto Devotha Malole
aliyefichwa chini ya uvungu wa kitanda kwa miaka mitano inaimarika na
kwamba bado anapatiwa matibabu.
Akizungumza jana, Dk Lyamuya alisema kwa sasa
mtoto huyo anasumbuliwa na vidonda vilivyopo kwenye makalio
vilivyosababishwa na kulazwa chini kwa muda mrefu pamoja na utapiamlo.
Alisema madaktari na wauguzi wamekuwa wakifuatilia
kwa karibu afya ya mtoto huyo ambaye yupo kwenye chumba cha uangalizi
wa karibu (ICU).
Dk Lyamuya alisema pamoja na matibabu mtoto huyo
bado anaendelea kupatiwa lishe ili kurudisha afya yake iliyosababishwa
na kukosa chakula bora kwa muda mrefu.
Dk Lyamuya alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Morogoro
Mjini, Abdulaziz Abood na Mkurugenzi wa Kampuni ya Alsaid, Omary Alsaid
kwa kuwa tayari kumsaidia mtoto huyo .
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paul
alisema polisi wanaendelea na uchunguzi na mtuhumiwa atafikishwa
mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Post a Comment