0

 
LIGI Kuu Italia imenasa kitu kimoja kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zilizofanyika nchini Brazil.
Teknolojia ya waamuzi kutumia vinyunyizo vinavyotoweka kwa haraka ili kutambua eneo lilipofanyika faulo na mahali ambapo wachezaji wanapaswa kujipanga kuweka ulinzi.
Waamuzi wote kwenye fainali za Kombe la Dunia la Brazil walitumia teknolojia hiyo. Kutokana na kuvutiwa na jambo hilo, Ligi Kuu Italia (Serie A) na Ligi Daraja la Kwanza (Serie B) zimeamua kuiga teknolojia hiyo na kwamba wataitumia kwenye ligi yao msimu ujao.
Hata hivyo, wakati Serie A ikijinadi kuiba teknolojia hiyo kutoka kwenye Kombe la Dunia, mikikimikiki hiyo itatibua hali ya mambo kwenye ligi hiyo kwa msimu ujao kutokana na nyota wake wengi waliong’ara nchini Brazil kutakiwa na timu za ng’ambo na hivyo huenda wasiwepo kwenye Serie A tena.
Jambo kama hilo limekuwa likitokea mara kwa mara kila inapofanyika michuano mikubwa kwamba kwa wachezaji waliong’ara wanaweza kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine, lakini kwa Italia ambayo klabu zake zinataka kujipanga ili kurejea makali yao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kitendo cha kuondokewa na wakali wake ni pigo.
Ligi Kuu Hispania ilitamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita kwa sababu klabu zake zinavutia wachezaji makini. Jambo hilo ni sawa na Ujerumani.
Kwa misimu kadhaa iliyopita, Ligi Kuu England ilikuwa ikitesa kabla kukumbwa na tatizo la kuondokewa kwa wakali wake na hivyo klabu za nchi hiyo kuanza kukumbana na wakati mgumu kwenye michuano ya Ulaya.
Sasa zinajipanga kujiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao huku Serie A ikiwa kwenye hatari zaidi kutokana na wachezaji wake nyota ambao wanafanya ligi ya nchi hiyo kuwa na mvuto kuwindwa na timu za nje.
Mauricio Isla
Kwenye umri wa miaka 26, Isla alionyesha kiwango kikubwa kwenye Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Chile. Klabu yake ya Juventus inaonekana kama haimtaki, lakini ukweli mchezaji huyo si wa kuachwa aondoke kirahisi.
Juventus haimtendei haki kwa sababu tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2012, Isla hakucheza mechi nyingi na hilo linamfanya staa huyo wa zamani wa Udinese kufikiria kuitema Serie A na kwenda kusaka ulaji kwingine.
Isla ni mpambaji wa kweli ndani ya uwanja. Anakimbia bila kuchoka na ni jambo la kawaida anapocheza kwa dakika tisini kuona anakimbia zaidi ya Kilomita 11. Kwa mujibu wa Fifa, faida ya kuwa na Isla kikosini ni kwamba anasaidia kwenye ulinzi na kushambulia.
Alikuwa nguzo imara kwenye mtindo wa soka la kushambulia uliokuwa ukitumiwa na Chile kwenye fainali za Kombe la Dunia. Pia ni mchezaji ambaye makocha wamekuwa wakiwatumia kwa maelekezo maalumu ndani ya uwanja. Alitumwa kumtuliza Neymar, akatulia.
Paul Pogba
Juventus inataka kuibakiza silaha yao hiyo makini, lakini kwa kiwango kilichoonyeshwa na kinda huyo wa Kifaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia na kwenye Serie A msimu uliopita, ni wakati tu haujafika kumshuhudia nyota huyo kwenye jezi za timu nyingine.
Timu nyingi zinamtolea macho Pogba. Lakini, kuondoka kwake ni pigo kwa ligi ya Italia, kwa sababu ni wazi linapokuja suala la kutaja mastaa wa ligi hiyo, Pogba ni miongoni mwa majina hayo.
Akiwa na umri wa miaka 21 tu, tayari Pogba anatazamwa kama moja ya viungo makini zaidi duniani. Klabu za Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Paris Saint-Germain zote zinafukuzia saini ya staa huyo.
Jose Mourinho wa Chelsea ameripotiwa kutenga Pauni 60 milioni kwa ajili ya kumng’oa Ufaransa huyo kwenye Serie A na kumrudisha kwenye Ligi Kuu England.
Juan Cuadrado
Kulikuwa hakuna wasiwasi wowote wa kwamba Juan Cuadrado angeweza kuihama Fiorentina, lakini baada ya kiwango maridadi alichokionyesha kwenye Kombe la Dunia nchini Brazil akiwa na kikosi cha Colombia, wasiwasi sasa umekuwa mkubwa.
Kabla ya Kombe la Dunia alikuwa ni mchezaji anayefahamika ndani ya Serie A pekee. Nje ya hapo hakukuwa na nchi nyingine iliyokuwa ikimfahamu mchezaji huyo. Lakini, sasa amekuwa staa mpya wa dunia na anazivutia timu nyingi.
Mchezaji mwenzake kwenye kikosi cha Colombia, James Rodriguez ametesa sana kwa kuandikwa na magazeti. Si kama hakustahili, isipokuwa kinda huyo wa AS Monaco alifaidika sana kwa kucheza sambamba na Cuadrado kwenye fainali hizo za Brazil.
Cuadrado, hakika ndiye aliyeifanya Colombia kutesa kwenye fainali hizo. Ni mchezaji mwepesi sana, ana kasi, mtaalamu wa kukokota mipira na fundi wa kutengeneza nafasi za kufunga. Hilo lilikuwa na faida kubwa kwa Rodriguez na hatimaye akafunga mabao sita na kuibuka Mfungaji Bora kwenye fainali hizo.
Msimu uliopita alipangwa nafasi zote za pembeni. Kuna wakati pia alitumika kama kiungo wa kati, kiungo mshambuliaji na pia aliwahi kuchezeshwa kama straika. Cuadrado ni kiraka. Hivyo, kuondoka kwenye Serie A ni pigo kubwa kwenye ligi hiyo.
Arturo Vidal
Kiungo wa Chile, Arturo Vidal, anatajwa kuwa mchezaji bora duniani kwenye nafasi yake anayocheza. Kama atatangaza kuhama klabu nyingi zitapigana kuinasa saini yake.
Vidal, 27, aliwasili kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil akiwa majeruhi, lakini alipona kwa haraka na kuonyesha makali yake kwenye michuano hiyo.
Mwenyewe amesema atabainisha hatima yake ya msimu ujao wakati atakaporejea Italia akitokea kwenye likizo baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia.
Klabu ya Manchester United inamtaka na inaamini atakuwa staa wao mpya katika kipindi cha wiki tatu zijazo japo kwamba Liverpool nao wameingia vitani kwenye kumsaka nyota huyo.
Baada ya kuwa na pesa zilizotokana na mauzo ya Luis Suarez aliyekwenda Barcelona, Liverpool sasa anajiona wana nguvu ya kusajili kila mchezaji aliyepo mbele yao. Wanamtaka Vidal na Pogba.
Mario Balotelli
Mario Balotelli hakucheza vizuri sana kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Brazil. Hata hivyo, kikosi cha Italia kwa ujumla hakikuwa kizuri wakati wa fainali hizo.
Balotelli alikwenda kwenye fainali hizo akiwa kwenye presha kubwa. Hakufanya vizuri, lakini hilo halimzuii kuwindwa na timu mbalimbali zinazohitaji saini yake.
Kabla ya fainali za Kombe la Dunia
straika huyo wa AC Milan alihusishwa na mpango wa kujiunga na Arsenal. Baadaye mambo yakagoma.
Aliporejea kutoka kwenye michuano hiyo miamba ya soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain ilitajwa kuwania saini ya mchezaji huyo huku Jose Mourinho na kikosi chake cha Chelsea akipiga hesabu kali za kumnyakua.Kuondoka kwa Balotelli kwenye Ligi Kuu Italia ni pigo kwenye ligi hiyo kutokana na ukweli kwamba mkali huyo ni moja ya nyota wanaolitambulisha soka la nchi hiyo. Agosti kitakuwa kipindi kigumu sana kwenye Serie A kutokana na klabu zake kuwa kwenye wakati mgumu wa kupambana kuwabakiza nyota ili wasihame. Wengi wao walio kwenye hatari ya kuhama ni wale waliotikisa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.

Post a Comment

 
Top