0

“Unakuta kwenye vyama tunazalisha tani 445 za korosho halafu unapata sulphur tani 22 badala ya tani 100. Hii ndiyo sababu ulanguzi upo kutokana na pembejeo kidogo zinazoletwa na Serikali. Kama pembejeo za ruzuku zingekuwa zinatosha tusingekuwa tunalia na mfuko wa pembejeo,” anasema Mchola.PICHA|MAKTABA  

“Wakulima wa korosho tunaweza kuboresha uchumi wetu kama Serikali itakuwa na nia madhubuti ya kukuza na kuwekeza katika kilimo.”
Hayo ni maneno ya mkulima wa korosho wilayani Tandahimba, Chiboko Ally (65). Anasema kuwa kama mkulima akiwekeza kwenye kilimo na kuungwa mkono na Serikali, lazima uchumi utakua.
Kwa mujibu wa Ally, ni vigumu kwa mkoa kama Mtwara kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia ardhi kwa kutegemea zao la korosho licha ya kuwa ndiyo zao tegemezi kwa wananchi wake kwani mara nyingi pembejeo zimekuwa zikicheleweshwa.
Hata hivyo, yapata wiki moja tangu mfuko wa kuendeleza zao la korosho nchini (CIDTF), kuzindua rasmi ugawaji na usambazaji wa pembejeo za ruzuku kwa msimu wa mwaka 2014/ 2015, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wakulima wakisema ugawaji wa pembejeo umekuwa kitendawili kutokana na upatikanaji wake kuwa mgumu.
Mkulima huyo anasema kuwa amekuwa akitegemea zaidi pembejeo za ruzuku kutokana na bei yake kuwa na nafuu licha ya kuwa hazikidhi mahitaji ya mkulima na kwamba wamekuwa wakiumia zaidi hasa linapokuja suala la upuliziaji na maandalizi ya shamba.
Anaeleza kuwa amekuwa akijikita kwenye kilimo hicho kwa miaka mingi hata kabla ya kuanzishwa kwa mfuko wa kuendeleza zao la korosho nchini ambao unahusu zaidi ruzuku. malengo ya mfuko huo yalikuwa ni kufanya mabadiliko kwa mkulima ili aweze kupata pembejeo za kutosha na pia kuvuna kwa mafanikio.
“Nimezaliwa katika familia inayojihusisha na kilimo cha korosho na kukulia katika zao hili kabla hata ya kuanzishwa kwa mfuko huu wa pembejeo, lakini bado haujaleta mabadiliko ya kuridhisha kwa mkulima licha ya kuwa na malengo mazuri,” anasema Chiboko.
“Wito kwa Serikali ni kwamba iongeze zaidi pembejeo ikiwezekana kutoa zaidi ya mara moja kwa msimu mmoja kwani kwa sasa mfuko hutoa mara moja tu kwa msimu.”
Uhaba wa pembejeo
Kwa upande wake, Mlela Mlela ambaye ni mkulima wa zao hilo, anasema mfuko wa pembejeo za ruzuku haujavutia, kwani mawakala wanaosambaza pembejeo hizo wamekuwa wakiwapelekea wakulima kiasi kisichotosha na kujikuta wakiwa kwenye wakati mgumu pindi wanapofanya maandalizi ya kupulizia mikorosho.
Anaeleza kuwa unaweza kukuta mkulima anamiliki shamba la ekari 20 halafu anapatiwa mifuko 10 ya pembejeo. Hiyo haikidhi haja, hivyo kuwalazimu kununua nyingine kutoka kwa matajiri ambao huwauzia kwa bei ya juu hali ambayo inazidi kuwadidimiza kiuchumi.
“Pembejeo hazikidhi mahitaji ya mkulima hata kidogo. Unakuta mkulima una shamba la ekari 20, lakini unapatiwa mifuko 10 ambayo haikidhi mahitaji na kutulazimu kununua nyongeza toka kwa machuuzi ambao hutuuzia kwa bei ya Sh25,000 hadi Sh30,000 kwa mfuko wa kilo 25 tofauti na zile za ruzuku ambazo kwa mfuko wa kilo 25 bei yake inakuwa Sh15,000” anaeleza Mlela.
“Hali hiyo imekuwa ikizidi kutudidimiza wakulima kiasi kwamba malengo yetu ya mwanzoni mwa msimu, hayatimii ikitokea hali hiyo na kusababisha tuishie pabaya,” anasema Mlela.
Naye Arab Mchola, mkulima ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika (Amcos) anasema kuwa kiasi kidogo cha pembejeo wanachopatiwa wakulima, hakifanani na hali halisi na hivyo husababisha kuwe na ulanguzi kutokana na mahitaji ya Serikali kuwa madogo.
“Unakuta kwenye vyama tunazalisha tani 445 za korosho halafu unapata sulphur tani 22 badala ya tani 100. Hii ndiyo sababu ulanguzi upo kutokana na pembejeo kidogo zinazoletwa na Serikali. Kama pembejeo za ruzuku zingekuwa zinatosha tusingekuwa tunalia na mfuko wa pembejeo,” anasema Mchola.
Muda wa ugawaji wa pembejeo
Hata hivyo, malalamiko ya wakulima hao kutopata pembejeo kwa wakati, ilimfanya mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia kuagiza wapatiwe pembejeo kwa wakati unaotakiwa.
Aidha, Yusuph Ally, mkulima wa korosho kutoka Wilaya ya Tandahimba, anasema kuwa Serikali inatakiwa kuwasaidia wakulima wapate pembejeo kwa wakati ili kupata mazao mazuri na kupunguza umaskini kwani ndilo zao pekee linalotegemewa na wananchi walio wengi.
“Kuchelewa kwa pembejeo kunaathiri upatikanaji mzuri wa mazao kwani inatakiwa wakati wa upuliziaji mkulima awe na pembejeo za kutosha, lakini kwa hili limekuwa tofauti, licha ya kuwa korosho ndiyo zao linalotegemewa zaidi hasa katika mkoa huu,” anasema Ally
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho nchini, (CIDTF), Suleiman Lenga, akizungumza wakati wa ufunguzi wa pembejeo za ruzuku msimu wa mwaka 2014/ 2015, anasema kuwa majukumu ya mfuko huo ni kuendeleza kilimo cha korosho kwa kusaidiana na Bodi ya Korosho na pia umekuwa ukigharamia mafunzo ya wakulima na waghani kwa ajili ya utafiti na dawa.
Lakini, Lenga anasema ugawaji wa pembejeo umeanza hata kabla ya ufunguzi na kwamba msimu wa mwaka 2013/2014 haukufungwa na kuwataka wakulima kulipa kiasi cha Sh15,000 kwa mfuko wa kilo 25 ili kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji na kwamba pembejeo zipo za kutosha.
“Lengo la Serikali ni kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji kwani pembejeo zipo za kutosha hivyo mawakala wahakikishe pembejeo zinamfikia mkulima kwa wakati na kwa gharama iliyopangwa na hivyo wakulima wasikubali kununua pembejeo isiyo ya ruzuku,” anasema Lenga.
“Pembejeo za ruzuku hutolewa kwa wakulima kulingana na mahitaji kutoka kwa maafisa kilimo wa ngazi ya wilaya ambayo nao huyapata kutoka kwa wagani wa kata ambao huzigawa kwa mujibu wa fedha zilizopatikana kutokana na bajeti ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo.
“Hatuwezi kusema kwamba pembejeo za ruzuku ni chache kwani huwa tunapokea mahitaji ya wakulima kupitia kwa maofisa kilimo wa wilaya husika. Ndani yake kuna maofisa ugani kutoka katika kata na pembejeo huwa tunazigawa kwa mujibu wa pesa tulizopata kwa mujibu wa bajeti iliyopo ambayo hutolewa na Serikali,” anasema Lenga.
Hata hivyo, ofisi yake imekuwa ikiishauri Wizara ya Kilimo kuongeza bajeti ya ununuzi wa pembejeo hizo za kilimo cha zao la korosho ili kuinua zao hilo hapa nchini.
“Tumeiomba Serikali kuongeza bajeti ya pembejeo ili kuweza kuwafikia wakulima wengi zaidi ili tufikie malengo yetu ya kimkakati tuliyojiwekea” anasema Lenga.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanawalalamikia watu wanaohusika na pembejeo kwamba baadhi yao wamekuwa wakinufaika na pembejeo kwa kuuza kwa bei ya juu.
“Tunaishauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka makao makuu kupitia namna pembejeo zinavyouzwa hovyo hapa Mtwara. Wananchi wengi hatutendewi haki, hali ni mbaya sana,” anasema mmoja wa wakulima ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa sababu za kiusalama

Post a Comment

 
Top