0
Emmanuel Okwi.PICHA|MAKTABA

MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji amevunja ukimya na kujibu tuhuma zote zinazoikabili klabu, lakini akampa masharti mawili Emmanuel Okwi raia wa Uganda anayeshinikiza uongozi ummalizie dola zake 40,000 za usajili ili aendelee na kazi.
Yanga ilimsajili Okwi kwa ahadi ya kumpa dola 100,000 lakini ikampa dola 60,000 na kuahidi kumalizia baadaye. Manji amesema, Okwi alisajiliwa klabuni hapo kwa mkataba wa miaka miwili na nusu na walikuwa na makubaliano ambayo moja kati ya jukumu lake ilikuwa ni kufuatilia kibali cha kumruhusu kucheza mpira Yanga.
Lakini kibali hicho kilichelewa akakosa baadhi ya mechi za awali, pia akajitoa kwenye timu bila ruhusa maalumu hivyo anachotakiwa ni kukatwa sehemu ya pesa zake za usajili au aongezewe muda wa usajili uwe miaka mitatu.
“Majadiliano na Okwi yanaendelea tutakachokubaliana na ndicho kitafanyika. Kama ilivyokuwa malengo yetu, tulimsajili mchezaji huyo kwa ajili ya mashindano ya kimataifa,”alisema Manji ambaye hana masihara linapokuja suala la fedha za klabu.
Kiongozi huyo atalitolea ufafanuzi zaidi suala la yeye kutogombea Juni Mosi mwaka huu kwenye mkutano wa kurekebisha katiba utakaofanyia Ukumbi wa Oysterbay Police Mess  na mpango wake ni kuwa, uchaguzi ufanyike Juni 15, mwaka huu.
Akitolea ufafanuzi suala la uchaguzi kuwahi, Manji alisema; “Nimefanya hivi kwa ajili ya kutoa nafasi katika usajili. Unajua kama tutachelewa na uongozi wa sasa ukafanya usajili inaweza kuwa tatizo kwa mwingine unaokuja labda wachezaji tutakaowasajili sisi litakuwa siyo chaguo lao.”
Kuhusu Domayo, Kavumbagu
Amesema, tangu Aprili hakuwepo nchini lakini amesikia maneno mengi yanazungumzwa kuwa wamefanya uzembe kuwapoteza wachezaji wawili, Frank Domayo na Mrundi Didier Kavumbagu.
“Ukweli ni kwamba, suala la Kavumbagu ilijulikana awali msimu huu wachezaji wa kigeni ni watatu tu na tuliuliza TFF lakini tatizo likaja, wakati tunajibiwa Kavumbagu alikuwa tayari amesajiliwa na Azam,”alisema Manji na kusisitiza Kavumbagu alikuwa mchezaji mzuri lakini watapata mwingine mzuri zaidi ya huyo.
“Kuhusu Domayo, kweli ni kijana mdogo tulifanya uzembe kidogo hata hivyo, amekwenda Azam lakini atarudi Yanga kama ilivyokuwa kwa Mrisho Ngassa.
Lakini akaenda mbali na kutupa dongo la baadhi ya viongozi ambao wanaponda juu ya hilo wakati wao ndiyo wana matatizo makubwa.
“Nimeongoza kwa miezi 19 lakini wapo walioongoza nyuma yangu lakini hawakufanya kama mimi, walikuwa wanakimbia wanachama na kutoitisha mikutano na wengine wanagombea uchaguzi mbalimbali lakini wanashindwa.
“Nimesikia wanachama wanamfuata mwanachama mmoja awasaidie kuongoza, kweli Yanga mmekosa wa kuwaongoza? Huyo mnayemfuata tumemwandikia barua ya kulipa pesa za ahadi ya gari la usajili wa Ngassa (Mrisho) ambayo alidai kutoa lakini hadi leo hii hajailipa,”alifafanua Manji na kueleza juu ya kocha wao Mholanzi Hans Van Pluijm kuwa kabla ya kuja Yanga walijua ataondoka.
“Nashangaa kauli ya kusema tunajenga uwanja kwenye maji itakuwaje. Ndiyo tunapopataka hapohapo, tunayo mifano ya viwanja vya nchi zilizoendelea kama Dubai, Uholanzi ambao wamejenga juu ya maji kwa nini sisi tushindwe,”alihoji na kutolea mfano mwaka 1964 Serikali yenyewe ilikuwa na mpango wa kujenga Uwanja wa Taifa hapohapo Jangwani.
Manji pia ametimua wanachama sita na kulifuta tawi la Tandale. Wanachama Haji Kamtange, Waziri Jitu, Athuman Matandula, Islael Dude, Mohamed Ndomba na Seleman Hassan ndiyo waliofutwa uanachama kwa sababu walizungumza na vyombo vya habari kinyume na taratibu.
Pia amelifuta tawi la Tandale ambalo linachochea vurugu na uvunjaji amani kwenye klabu.

Post a Comment

 
Top