Okocha
ATIKA dimba la Uwanja wa Taifa wa Ufaransa, maarufu kama Stade
de France, Juni 28, 1998, Watanzania walikuwa wameganda katika luninga
zao wakishindwa kuamini kuwa timu ya Afrika waliyokuwa wanaishabikia
katika Kombe la Dunia ilikuwa imekufa kwa mabao 4-1 kutoka kwa Denmark.
Ndio, kama ilivyo kwa Waafrika wengine, Watanzania
walikuwa wamejipa ushabiki wa timu ya Taifa ya Nigeria. Lakini Peter
Moller akaipatia Denmark bao la kwanza. Brian Laudrup akaipatia bao la
pili, Ebbe Sand akaipatia la tatu, Thomas Helveg akaipatia la nne.
Dakika mbili baadaye, Tijani Babangida akaipatia Nigeria bao la kufutia
machozi.
Kwanini Watanzania tulikuwa mashabiki wa Nigeria?
Kwanza kabisa walikuwa wametukosha katika fainali za Kombe la Dunia
mwaka 1994 nchini Marekani. Pili wakatukosha kwa kutwaa medali ya
dhahabu ya Olimpiki pale Atlanta Georgia Marekani.
Hata baada ya kupigwa na Denmark Watanzania
wakaendelea kuwa mashabiki wa Nigeria. Mpaka leo bado wapo mashabiki wa
Nigeria nchini. Mashabiki wa damu. Lakini unadhani Wanigeria wana
tofauti kubwa kisoka na sisi? Hapana.
Wanigeria wanajituma katika kuhaha kutafuta
maisha. Taifa lao lina watu zaidi ya milioni 170 kwa sasa. Kila Mnigeria
anajituma kadri anavyoweza. Huyu anatapeli, yule anacheza soka, huyu
anaimba, mwingine anaanzisha dhehebu feki la dini. Ili mradi mkono uende
mdomoni.
Na ni kwa njia hii ndio Wanigeria wametugeuza kuwa
mashabiki wao. Vipaji vya wachezaji wao ni hivi hivi vya wachezaji
wetu. Tofauti ni katika kutafuta maisha. Yakubu Aiyegbeni ndiye Edward
Chumilla. Waliomwona Sunday Manara hawamtofautishi sana na Jay Jay
Okocha.
Peter Rufai alikuwa kipa wa kawaida asiyefikia
uwezo wa Mohamed Mwameja wala Riffat Said. Hata mabao manne waliyofungwa
na Denmark alichangia kiasi kikubwa kufungisha.
Baada ya soka lao, Watanzania tulihamia katika
filamu zao. Mama zetu, dada zetu na watoto zetu wakahamia katika kupenda
filamu za Kinigeria. Ukweli ni kwamba hawakuwa na jipya sana ambalo
sisi hatukuwa nalo.
Mastaa wao Nouah Ramsey, Desmond Elliot, John
Okafor, Ini Edo na wengineo wana vipaji ambavyo Tanzania vilionekana
tangu zama za akina Bishanga na wengineo. Tatizo ni uwezo wa Wanigeria
kubuni vitu viwili vitatu kama vile kuingiza mambo mengi ya kishirikina
ambayo tulikuja kuyaiga.
Hata hivyo maudhui yao ni yale yale ya kawaida
ambayo wacheza filamu wetu wameyazoea. Mara nyingi unakuta mtoto wa
tajiri amempenda masikini. Hakuna jipya sana, hakuna sehemu ambayo
wanaweza kuangusha ndege kama Hollywood wanavyofanya na filamu zao za
kusisimua.
Tatizo hapa wacheza filamu wetu hawajitumi. Wengi
hawana vipaji wala elimu. Wanacheza filamu kwa sababu walikuwa Mamiss,
wanamitindo au wamerudi kutoka katika Shindano la Big Brother.
Vinginevyo hatuangalii vipaji. Tunaangalia wauza sura.
Matokeo yake tumejikuta tukirudi kuwa mashabiki wa
Filamu za Kinigeria bila ya sababu za msingi. Hakuna unachoweza kufanya
zaidi ya kucheka. Mcheza filamu yuko bize na matajiri kuliko kujikita
katika kazi yake apate pesa za kuwa tajiri.
Hata hivyo kama vile haitoshi, baada ya Wanigeria kutuchukua
kutoka katika soka na filamu, sasa wametuteka katika muziki. Nenda
katika baa maarufu popote Tanzania, au nenda katika ukumbi maarufu wa
disko ukasikie jinsi nyimbo za mwanamuziki Davido wa Nigeria
zinavyotuteka.
Wimbo wake wa Aye kwa sasa ni kama wimbo wa taifa
wa muziki. Kabla ya hapo wimbo wake wa Skelewu ulikuwa gumzo
lililopitiliza. Lakini ukichunguza sana katika nyimbo zake, hakuna cha
ajabu ambacho Watanzania hawawezi kufanya.
Wimbo wa Aye unamuonyesha akiwa shambani. Lakini
kama Diamond Platinumz akipiga nyimbo inayomuonyesha akiwa mashambani
watu watapuuza. Hata yeye mwenyewe hataki. Aliwahi kufanya wimbo mmoja
akiwa kijijini, lakini haukuvuma.
Ndio maana sasa anafanya video za kifahari Afrika
Kusini, anaonekana akirekodiwa kutoka angani na vifaa vya kisasa.
Kwanini Davido anatuteka zaidi ya Diamond? Kwanza ni kwa sababu ya
kupenda Unigeria ambao umetuingia.
Pili wenzetu wamefanikiwa kujitangaza kimataifa.
Vipaji ni vilevile tu, lakini kama P Square wanafanya wimbo na Ricky
Ross huku wewe unamtafuta Jackline Wolper na kujaribu kumfanya kuwa
mwanamuziki ili auze sura katika wimbo wako wakati hana kipaji chochote
cha muziki.
Muziki wanaoufanya Wanigeria tunaweza kuufanya.
Mimi ni mmoja kati ya watu wanaoamini hilo. Tatizo ni wanamuziki wetu
kukosa ubunifu, au Watanzania wenyewe kuwa wepesi katika mapokeo ya kila
kitu.
Post a Comment