Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
amebaini madudu ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
ambapo mikopo ilitolewa ni kwa wanafunzi waliofeli mitihani.
Kiasi cha Sh214.5 milioni kilitolewa kama mkopo
kwa wanafunzi walioshindwa mitihani na kutoendelea na chuo na wengine
walioahirisha masomo katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.
Taarifa ya CAG, Ludovick Utouh aliyoiwasilisha
Bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita, imebainisha wanafunzi walioacha
masomo au kuahirisha masomo kuwa nao waliendelea kupatiwa mikopo hiyo.
CAG amebainisha kuwa kitendo hicho kilikuwa ni
kinyume cha ibara ya pili, sehemu ya kwanza ya mwongozo wa ukopeshaji wa
HESLB inayoelekeza vigezo vya wanaostahili kupata mikopo.
Moja ya vigezo hivyo ni ufaulu kwa wanafunzi kuelekea mwaka wa masomo unaofuata.
Hata hivyo CAG alibaini kwa mwaka 2012/2013, HESLB
ilitoa mikopo ya Sh214.5 milioni kwa wanafunzi waliofeli au kuahirisha
masomo katika vyuo vikuu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya vyuo hivyo ni pamoja na vyuo vikuu
katika nchi za Algeria na Cuba ambazo wanafunzi wake walipewa mikopo ya
Sh131 milioni huku mikopo kwa wanafunzi Urusi ikiwa Sh9.6 milioni.
Nchini, wanafunzi waliopewa mikopo hiyo wanatoka
Chuo kikuu Dodoma (UDOM) walilipwa Sh43.9 milioni na Chuo cha Usimamizi
wa Fedha (IFM) walilipwa Sh28.9 milioni.
Post a Comment