WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais, asiyekuwa na wizara maalumu, Profesa Mark
Mwandosya, amempigia debe Spika wa Bunge, Anne Makinda, akisema kuwa
anafaa kuwa rais kutokana na sifa zake.
Profesa Mwandosya alimwaga sifa hizo bungeni jana, wakati akiunga mkono
Azimio la Bunge la kumpongeza Makinda, kutokana na kuchaguliwa kwake
kuwa Rais wa Chama cha Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola
(CPA).
Profesa Mwandosya, ambaye miaka ya nyuma alijitosa katika kinyang’anyiro
cha urais, alisema Spika Makinda ana sifa zaidi ya kumi ambazo
zinamtosheleza kuwa rais na kwamba ni watu wachache wenye sifa kama
hizo.
Akitaja sifa hizo, Profesa Mwandosya alisema Makinda ni mtu
anayejiamini, mtenda haki, mchapakazi, mzoefu, msikivu, mbunifu,
mwelewa, mvumilivu, mnyenyekevu na pia ni mtu mwenye msimamo.
Alisema kutokana na sifa hizo, Makinda anafaa kuwa kiongozi wa ngazi ya
juu katika nchi, huku akimtazama kuwa ni mwanamke tishio katika uchaguzi
mkuu ujao wa mwaka 2015.
“Kwa namna ninavyomfahamu Spika Makinda ni tishio kwa uchaguzi wa rais
mwaka 2015, kutokana na jinsi alivyokuwa na uwezo na mambo aliyowahi
kulifanyia taifa hili.
“Kuchaguliwa kwake kuwa rais wa CPA ni hatua muhimu na nzuri kwa
wanawake wengi kuongezeka katika Bunge la mwaka 2015 kwa kufikia
asilimia 55, kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka,” alisema Profesa
Mwandosya.
Profesa Mwandosya, ambaye amekuwa serikalini kwa muda mrefu, mwaka 2005
alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais.Hata
hivyo, kutokana na mchujo, Mwandosya alifanikiwa kuingia katika tatu
bora. Wengine walikuwa ni Dk. Salim Ahmed Salim, Rais Jakaya Kikwete.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), alimwaga sifa kwa
kiongozi huyo wa Bunge na kusema kuwa ni mwanamke shupavu atakayekuwa
tishio katika uchaguzi mkuu ujao.
Akichangia mjadala huo wa kumpongeza Spika, Anna Abdallah, alisema
Makinda ni mwanamke mwenye uwezo wa kuongoza nafasi yoyote ya juu,
ikiwemo urais wa nchi.
Alisema kutokana na uzoefu wake katika uongozi hapa nchini, ameweza
kuaminika hata nje ya nchi, jambo ambalo limemfanya kuchaguliwa kuwa
Rais wa CPA.
“Kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa ikihubiri juu ya mwanamke kupewa fursa
na hasa kama ana uwezo, sasa wenzetu CPA wameweza kuliona hili
wamemchagua,” alisema.
Mbunge huyo aliwataka wanawake kutojali maneno ya pembeni na sasa ni
lazima jamii ikubali kumuamini mwanamke kwa kumpa nafasi ya juu ya
uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Awali akisoma Azimio hilo la Bunge, Mwenyekiti wa CPA-Tanzania, Mussa
Azzan Zungu, alisema Spika Makinda alishika wadhifa huo baada ya
kufanyika kwa mkutano wa 44 wa chama hicho.
Zungu, ambaye ni Mbunge wa Ilala, alisema katika mkutano huo Bunge la
Tanzania liliwakilishwa na wabunge wanane, akiwemo Spika Makinda na
baadaye ulifanyika uchaguzi huo.
Chanzo:Mtanzania
Post a Comment