Dar es Salaam. Mwakilishi wa Timu ya Soka ya FC Lupopo ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ismael Balanga Bandua, amenusurika
kufungwa jela kwa kuishi nchini bila kibali, baada ya kutiwa hatiani na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa hayo.
Bandua ambaye alifika nchini hivi karibuni kwa
lengo la kukamilisha taratibu za timu hiyo kumsajili kipa wa zamani wa
Simba, Timu ya Taifa (Taifa Stars), Juma Kaseja alipatikana na hatia
hiyo jana baada ya kukiri kutenda makosa hayo.
Baada ya kusomewa mashtaka, Mkongo huyo alikiri kutenda makosa hayo, lakini akajitetea kuwa alikuwa hajui sheria za Tanzania.
Kutokana na kukiri kwake makosa hayo, Hakimu Mkazi
Hellen Riwa alimhukumu kifungo cha miezi mitatu jela, ama kulipa faini
ya Sh50,000.
Alinusurika kutupwa jela, baada ya kufanikiwa
kulipa faini hiyo ya Sh50,000 iliyochangwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni
ndugu zake walioko hapa nchini kihalali.
Alipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana na
kusomewa mashtaka ya kuishi nchini bila kibali kinyume cha kifungu cha
31(1)(i) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji, Sura 54, kama ilivyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Katika kesi hiyo, Wakili wa Uhamiaji, Patrick
Ngayomela, pia alidai kuwa Mkongo huyo anakabiliwa na shtaka la
kuwapotosha maofisa Uhamiaji.
Post a Comment