Osama bin Laden aliitikisa dunia, ingawa ni kwa kipindi kifupi
tu. Kwa kutumia kundi lake la Al Qaida, Osama alihusishwa kwenye
mashambulizi kadhaa mabaya sehemu mbalimbali duniani yaliyosababisha
vifo vya watu. Kubwa kuliko yote ni lile lililotokea Septemba 11, 2001,
nchini Marekani. Kutokana na hali hii Osama akawa mwanadamu anayesakwa
kwa udi na uvumba. Jina lake likawa maarufu kupita kiasi na waandishi
mbalimbali wakaandika makala, chambuzi na hata vitabu kumhusu. Kwenye
simulizi hii iliyotafsiriwa kwa Kiswahili na MIKI TASSENI, tunapata
mtiririko wa mambo jinsi yalivyopangwa na yalivyotokea hadi bin Laden
alipokamatwa na kuuawa akiwa katika maficho nchini Pakistan.
Jana tuliona jinsi al Qaeda ilivyokuwa ikifanya
mashambulio ‘ola’ na kusababisha vifo vingi vya Waislam, jambo ambalo
lilimhuzunisha sana Sheikh…
“Hapa kuna jambo muhimu ambalo tunatakiwa
kuliangalia: kufanya mashambulio kadhaa bila kuchukua tahadhari, ambako
kumeathiri hisia za makundi ya watu katika Taifa kuhusu mujahidin.
Itapelekea sisi kushinda mapambano kadhaa huku tunashindwa vita
mwishoni.
“Inahitaji mpangilio mzuri wa kila shambulio kabla
ya kulifanya, pia kupima faida na hasara zake, halafu kuamua ni
shambulio gani linafaa zaidi kufanya,” anaelekeza bin Laden.
Hata mafanikio yalimsumbua. Wakati wa mzingiro wa
Khobar, Saudi Arabia mwezi Mei 2004, kundi kubwa la magaidi lilichukua
mateka kutoka visima viwili vya mafuta na kuua wageni 19. Washambuliaji
hao walikuwa sehemu ya “Al Qaeda katika Ghuba ya Arabuni, tawi la Yemen.
Walikuwa wamewauliza mateka hao kila mmoja kama walikuwa Waislamu, na
kuchana makoo ya wale ambao hawakuwa Waislamu. Wengi kati ya watekaji
hao waliuawa katika operesheni ya uokoaji, na tukio hilo lilisaidia
kuanzisha kampeni katili ya serikali ya Saudia dhidi ya wafuasi wa siasa
kali.
Sheikh sasa alikuwa anaonya dhidi ya kufanya mashambulio kama hayo na mengineyo katika nchi za Kiarabu.
“Utawala uliopo utachukua hatua kali dhidi ya
mujahidin; hii itapelekea kujilinda wao wenyewe na kulipa kisasi kwa
utawala,” aliandika. “Ndugu wapiganaji na utawala watakuwa sasa katika
vita ambayo hatukuanzisha, kwa sababu nguvu ya ndugu wapiganaji haitoshi
kwa vita kama hiyo.
“Mkakati unaofaa ni kukwepa mapambano na serikali
za Kiarabu, kama Yemen, Iraq na Saudia, kukwepa kumaliza nguvu zetu
katika kukabiliana na serikali hizo katika kipindi hiki (na) kupoteza
hisia chanya za Waislamu kuhusu sisi. ..
Sisi ndiyo tunawalinda Waislamu na kupigana na adui yao mkubwa, umoja wa Makrusedi na Wazayuni.”
Ilikuwa inatosha sasa kuwa ‘watu kwa jumla’
wanaona kuwa wanaoathirika ni Waislamu, hata kama bin Laden, kwa viwango
vyake vinavyochuja zaidi, alikuwa hakubali hivyo. Kuwaua wanaoingia
katika kundi hilo, pamoja na kuweza kutetewa kimaadili, ilikuwa ni kosa
la kimkakati. Bora mashambulio ya baadaye yaje kutoka maeneo mbali na
Mashariki ya Kati, alisema. Alitaja Korea ya Kusini kama mfano.
“Kati ya nafasi za kutumia katika kuwalenga
Wamarekani ni hali dhaifu ya usalama inayoonekana katika nchi ambazo
hatujafanya mashambulio yoyote.”
Sheikh mara nyingi alikuwa anafundisha katika
barua zake, akijaribu kuuelekeza mtandao wake kuelekea katika malengo
yake makuu. Alikuwa na wasiwasi siyo tu kuwa matawi rasmi ya Al Qaeda
yalikuwa yanaambaa mbali na uelekezi wake, lakini malengo yake yalikuwa
yanavurugwa kwa kulenga vitu na mahitaji ambayo aliyaona hayana umuhimu.
Post a Comment