Na Mokongoro Oging'
Mkutano huo uliwajumuisha viongozi wa dini ya Kiislam, Kikristo na madiwani wa kata mbalimbali jijini Dar.
Akiongoza kikao hicho, Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Buguruni, ASP Batseba Kasanga kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Kipolisi Buguruni, Juliyo Simba alisema pamoja na mambo mengine waliazimia kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika nyumba za ibada.
Vikundi hivyo vinaanzishwa ili kudhibiti hali ya uvunjifu wa amani kupitia vivuli vya dini pia wamepiga marufuku mahubiri ya uchochezi.
Katika mkutano huo, viongozi wa dini walikatazwa kufanya mihadhara isiyokuwa na kibali cha polisi na walitakiwa kuwaelimisha waumini misingi ya dini zao.
Habari zinasema wote kwa pamoja walikubaliana kufanya mikutano ya mara kwa mara ili kuona kama yale waliyoyatathmini yanatekelezeka.
Askofu Laurence Kametta wa Kanisa la TAG Jimbo la Mashariki Kusini alisema katika mkutano huo kuwa kila kiongozi wa dini akihubiri kwa kufuata msingi wa kanisa lake au msikiti, hakuna ugomvi utakaotokea.
“Kufuta mihadhara siyo dawa kwani hata Yesu na mitume waliitumia pia inatusaidia kuwapata vijana wanaofanya maovu ambao hawajawahi kwenda msikitini ama kanisani baadaye wanaokoka na kujiunga nasi katika nyumba za ibada,” alisema Askofu Kametta.
Naye Ustadhi Abdi Bakari ambaye ni Katibu wa Kundi la Waislamu wa Tabata alisema kama kuna kikundi cha watu wanaotumiwa na wenye fedha kuleta vurugu nchini kwa misingi ya dini, serikali inatakiwa kuwashughulikia mapema ambapo alishauri mihadhara isifutwe.
Naye Diwani wa Kata ya Buguruni, Magina Lufungulo alisema kwamba kitendo kilichofanywa na jeshi la polisi la kuitisha mkutano wa viongozi mbalimbali wa dini ni cha kiungwana na alilikumbusha jeshi kuwa kioo cha jamii.
Post a Comment