Tume ya Mabadiliko ya Katiba juzi
ilizindua rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekeza mambo mengi ikiwa ni
pamoja na Uhuru wa habari na vyombo vya habari inayovitaka kusambaza
habari kwa kuzingatia utu, heshima na staha.
Rasimu hiyo inaeleza kuwa kila mtu anao uhuru wa kutafuta, kupata na kutumia habari na taarifa na kusambaza taarifa hizo.
Inafafanua kwamba masharti ya Ibara hiyo
yatalazimika kuzingatia masharti ya sheria ya nchi itakayotungwa kwa
ajili hiyo na kwa madhumuni ya kulinda usalama wa taifa, amani, maadili
ya umma, haki, staha na uhuru wa watu wengine.
“Kuanzisha vyombo vya habari na njia nyingine za
upashanaji wa habari bila kujali mipaka ya nchi, vyombo vya habari
vitakuwa huru na vilevile vitakuwa na haki ya kupata, kutumia na
kusambaza habari na taarifa” inaeleza rasimu hiyo.
Inafafanua kwamba vyombo vya habari vitakuwa na
wajibu wa kusambaza habari na taarifa kwa wananchi na kuheshimu na
kulinda utu, heshima, uhuru na staha ya wananchi dhidi ya habari na
taarifa wanazozitumia, wanazozitayarisha na kuzisambaza.
Inaeleza kuwa Serikali na taasisi zake, asasi za
kiraia na watu binafsi watakuwa na wajibu wa kutoa habari kwa umma juu
ya shughuli na utekelezaji wa shughuli zao. kufuatia hali hiyo baadhi ya
wadau wa habari wamesema rasimu ya katiba hiyo inaonyesha mwelekeo
mzuri wa utendaji kazi za habari nchini.
Wamesema kila nchi vyombo vya habari vyake
vinafanya kazi kwa kuzingatia masharti ya sheria inayolinda masuala ya
usalama wa taifa . Kwa kuzingatia hayo wamesema kinachotakiwa ni kuwapo
kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Post a Comment