Posted Jumanne,Juni5 2013 saa 22:26 PM
Kwa ufupi
Hakuna anayeweza kupinga ukweli kwamba
kupatikana kwa Katiba mpya ya Tanganyika ni jambo la lazima kabla ya
mwisho wa mwaka ujao, ili Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ikianza
kutumika mwaka 2015 Watanganyika nao wawe tayari wamepata Katiba yao
Baada ya Tume ya Marekebisho ya Katiba juzi kuandika historia
kwa kutoa rasimu ya awali ya Katiba mpya kwa kupendekeza mabadiliko
makubwa ya kimfumo na uendeshaji wa nchi yetu kwa siku zijazo, hatua
hiyo sasa imetengeneza ombwe upande wa Tanzania Bara, kwa maana ya
Watanganyika nao kuhitaji Katiba mpya kabla ya mwaka 2015.
Wazanzibari wanayo Katiba yao ya mwaka 1984 ambayo
ilifanyiwa marekebisho mwaka 2010. Hivyo, tunaweza kusema pasipo shaka
kwamba mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano hayatailazimisha
Zanzibar kuandika Katiba mpya, ingawa inaweza kufanya marekebisho ya
hapa na pale katika Katiba hiyo ya 1984 kwa lengo la kukidhi matakwa
mbalimbali yatakayotokana na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.
Hakuna anayeweza kupinga ukweli kwamba kupatikana
kwa Katiba mpya ya Tanganyika ni jambo la lazima kabla ya mwisho wa
mwaka ujao, ili Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ikianza kutumika
mwaka 2015 Watanganyika nao wawe tayari wamepata Katiba yao. Ni bahati
mbaya kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya ya Serikali ya Muungano
haukuwa umepangwa, bali ulianza ghafla kutokana na shinikizo la vyama
vya upinzani na asasi za kiraia.
Kwa maneno mengine, iwapo suala la kupata Katiba
mpya ya Jamhuri ya Muungano lingekuwa limepangwa na kupata mwafaka wa
kitaifa mapema, mchakato wa kupata Katiba hiyo nao ungeanza mapema
angalao mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kutokana na hali
hiyo, mchakato huo ulikuja kama jambo la dharura na ndiyo maana Tume ya
Warioba ililazimika kufanya kazi usiku na mchana kukusanya maoni ya
wananchi, kuyaratibu na kutoa rasimu ya awali ya Katiba mpya katika muda
mfupi.
Kwa kukubali shinikizo la vyama vya upinzani na
vuguvugu la mageuzi la kutaka ipatikane Katiba mpya kabla ya mwaka 2015,
Rais Jakaya Kikwete alionyesha busara, uzalendo na ujasiri wa hali ya
juu kwa sababu aliiepusha nchi yetu isiingie katika machafuko ya
kisiasa. Sote tulikuwa mashahidi wa jinsi viongozi wengi wa chama chake,
wakiwamo wabunge walivyokakamaa wakipinga kuandikwa kwa Katiba mpya,
huku baadhi wakitaka Katiba ya sasa iwekwe viraka tu.
Hivyo, ieleweke kwamba kuchelewa kuanza kwa
mchakato wa kupata Katiba mpya ya Muungano halikuwa tatizo la Rais
Kikwete. Ndani ya CCM ilikuwamo minyukano na mikikimikiki iliyotokana na
mifarakano ya kiitikadi na kisera ya muda mrefu, kwani wahafidhina
hawakutaka Katiba mpya kwa hofu ya kupoteza dola. Ni kwa sababu hiyo
Rais alionekana kusimama peke yake akitafuta mwafaka wa kitaifa kwa
kukutana na kupokea mapendekezo ya upinzani na asasi za kiraia kuhusu
Rasimu ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ambayo ingejadiliwa na
kupitishwa na Bunge, hivyo kuruhusu mchakato wa Katiba mpya kuanza.
Tumesafiri mwendo mrefu na kupita kwenye milima na
mabonde na kuweza kufika hapa tulipo. Sasa tunayo Rasimu nzuri ya awali
ya Katiba Mpya. Wakati mchakato huo ukiendelea, tungependa kumshauri
Rais Kikwete azindue mchakato mwingine wa kupata Katiba ya Tanganyika
ili ipatikane hata kabla ya Katiba ya Muungano. Rais amefanya kazi nzuri
mpaka sasa. Na huo ndiyo utakuwa urithi wake kwa Watanzania
atakapomaliza kipindi chake cha kuiongoza nchi yetu mwaka 2015.
.
Post a Comment