Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza
kuchunguza malalamiko ya Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbroad Slaa ya
kutaka kulishwa sumu na Mlinzi wake.
Madai hayo ambayo yamekuwa gumzo katika vyombo vya
habari wiki hii huku wananchi wakihoji uhalisia wake, yamemuhusisha
mlinzi huyo wa Dk Slaa huku yeye mwenyewe akikataa tuhuma hizo na kudai
kuwa ameteswa na walinzi wa chadema.
Kamanda wa kanda maalum ya Dar es Salaam Suleiman
Kova amesema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake kuhusu taarifa hizo zilizofikishwa katika kituo cha polisi
cha Oysterbey kupitia wakili wa Chadema John Malya ambae aliambatana
na mtuhumiwa Khalid Kagenzi (48) ambaye ni mlinzi wa Dk. Slaa ili
akatoe maelezo kwa niaba yake.
Mlinzi wa Dk. Slaa alidai kuwa ana majeraha
mwilini yaliyotokana na mateso aliyofanyiwa akiwa chini ya ulinzi mkali
wa maafisa wa usalama wa Chadema ambao walikaa naye na kumhoji kuanzia
tarehe 07/03 saa tano asubuhi hadi tarehe 08/03 mwaka huu saa kumi
jioni.
Aidha Kamanda Kova amesema kuna mambo mawili
yanafanyiwa uchunguzi likiwemo la mlinzi Khalid Kagenzi na la pili ni
dhidi ya watuhumiwa wanaodaiwa kumtesa kwa kumshambulia mlinzi huyo na
kumsababishia majeraha mwilini mwake.
Kova aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa na Jeshi
la Polisi kwa kosa la shambulio la kudhuru mwili ni Boniface Jacob,
(32) mkazi wa kisiwani Ubungo, ambae ni diwani kata ya Ubungo kupitia
Chadema,Hemed Ally Sabula (48) mkazi wa Tandale kwa Tumbo ambae Afisa
Usalama wa Chadema,Benson Mramba (30)mkazi wa Tabata Kisukuru ,Afisa
Utawala wa Chadema.
Aliongeza kuwa watuhumiwa hao watatu wapo chini ya
ulinzi kwa makosa yaliyotajwa dhidi ya Khalid Kagenzi na shauri
litafikishwa mahakamani kupitia kwa wakili wa serikali ili
kujiridhisha kisheria na hatimaye kutoa maamuzi kuhusu mashtaka yao.
Post a Comment