Dar es Salaam. Jukwaa la Wakristo Tanzania limewataka waumini
wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura,
kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya
“hapana”.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa hilo jana na
kusainiwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk
Alex Malasusa, mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki
Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na mwenyekiti wa Kanisa
la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet, imetaja sababu mbili
za uamuzi wake kuwa ni muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya
Taifa kuwa na Serikali isiyo na dini, na Kura ya Maoni kusababisha
mgawanyiko.
“Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote
wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya
elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi
kupiga kura ya hapana kwa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu zilizotajwa
hapo juu,” linasema tamko hilo la kurasa nne.
Taarifa hiyo imekuja siku moja tu baada ya Waziri
Mkuu Mizengo Pinda kutangaza kuwa muswada wa uanzishwaji wa Mahakama ya
Kadhi uliokuwa umeondolewa kwenye mkutano uliopita wa Bunge kwa ajili ya
mashauriano zaidi, utawasilishwa katika vikao vya chombo hicho
vinavyoanza Jumanne ijayo baada ya kufikiwa kwa maridhiano baina ya
viongozi mbalimbali wa dini.
Pia tamko hilo limekuja siku chache baada ya Rais
Jakaya Kikwete kuiagiza Hazina itoe fedha kwa Tume ya Uchaguzi (Nec) kwa
kadri inavyohitaji ili kuiwezesha kukamilisha mchakato wa Kura ya
Maoni.
Viongozi wa Jukwaa la Wakristo walikutana Machi
10, mwaka huu kujadili kwa kina kuhusu hali ya usalama wa nchi ilivyo
sasa na mustakabali wake, Katiba inayopendekezwa na uanzishaji wa
Mahakama ya Kadhi.
Katiba inayopendekezwa
Taarifa hiyo ya maneno 712 inasema: “Katiba
Inayopendekezwa imeleta mgawanyiko mkubwa katika Taifa kwani imepatikana
kwa njia zisizo za kiadilifu na mchakato wake umeendeshwa kwa hila na
ubabe.
“Pia haijajibu matakwa na malalamiko ya wananchi
kwenye masuala mbalimbali kama muundo wa Serikali, miiko na maadili ya
viongozi wa umma, haki za binadamu, madaraka ya rais na uwiano wa
mihimili ya dola.
“Ikumbukwe Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa
kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwa ahadi ya Serikali kuipa dini ya
Kiislam Mahakama ya Kadhi. Inashangaza kuwa hata Serikali inatoa rushwa
ili kufikia malengo yake. Kwa hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga
mkono kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa,” ilisema sehemu ya tamko
hilo.
Mahakama ya Kadhi
Kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, taarifa
hiyo inasema, “Suala la uanzishwaji wa Mahakama hii nchini kama
tulivyotoa maoni yetu kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria (Januari
16, 2015); barua yetu kwa Waziri Mkuu na matamko mbalimbali yaliyokwisha
kutolewa kuhusu jambo hili; Mahakama ya Kadhi inakiuka misingi ya Taifa
hili kuwa na Serikali isiyokuwa na dini wala mfumo wa sheria unaobagua
raia wake kwa misingi ya dini.”
Inaeleza kuwa mjadala unaoendelea unavunja Katiba ya Jamhuri
Ibara ya 19 kwa kuendelea kujadili suala hilo katika Ilani za vyama vya
Siasa, majukwaa ya kisiasa na bungeni na kusisitiza kuwa suala hilo
limeligawa Taifa, Serikali, Bunge, Mahakama na wananchi.
“Mahakama ya Kadhi imekuwa ikiendelea kutumiwa na
wanasiasa kama mtaji wao wa kujipatia madaraka kwa gharama za kuleta
chuki za kidini.
“Kwa dhamiri safi, Jukwaa linatamka wazi kuwa
mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya kidini kuhusu
uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria ufungwe na badala
yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya masuala hayo bila
kuihusisha Serikali wala waumini wa dini nyingine,” inasema taarifa
hiyo.
Hali ya usalama
Kuhusu hali ya usalama nchini Jukwaa hilo
limeeleza kusikitishwa na viashiria pevu vya ugaidi vilivyoanza
kujitokeza nchini kwa takribani miaka mitano iliyopita na kwamba
kumekuwa na vitendo vinavyoashiria kuchipuka kwa ugaidi nchini.
Maaskofu hao wameyataja matukio kama vile uvamizi
wa vituo vya polisi, kuporwa silaha na mauaji ya polisi, mafunzo ya
kareti katika nyumba za ibada, mafunzo ya itikadi kali za kidini kwa
watoto, tukio la Amboni Tanga, mauaji ya viongozi wa dini, uchomaji wa
nyumba za Ibada na kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa dini.
“Jukwaa linasikitishwa na mwendelezo wa mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino) na ukatili unaosababisha ulemavu
wa kudumu wa maalbino katika nchi yetu. Hali hii inatishia utulivu,
amani na umoja wa kitaifa tuliokuwa nao kama Taifa la mfano barani
Afrika,” inaeleza taarifa hiyo.
Jukwaa hilo limewataka wananchi kuacha tabia ya
kuua albino na kusisitiza kuwa kukosekana kwa uwajibikaji wa viongozi wa
Serikali na kuongezeka kwa wigo wa kipato kati ya walionacho na
wasionacho kunachangia ongezeko la vitendo hivyo viovu.
“Mbona tembo na ng’ombe wakiuawa operesheni
maalumu zinafanyika na viongozi wanawajibika, kwa nini maalbino wakiuawa
viongozi hawawajibiki,” inahoji sehemu ya taarifa hiyo.
“Kwa kuwa chama tawala na Serikali wameshindwa
kusimamia misingi iliyolea taifa kama serikali isiyo ya kidini na taifa
lenye amani; umoja na utulivu; Jukwaa linawaelekeza waumini wote na
wenye mapenzi mema wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao kufanya maamuzi
yanayolitanguliza Taifa badala ya kutanguliza mazoea, mapokeo, itikadi
na ushabiki wa chama fulani cha Siasa.”
Post a Comment