0
Unapozungumzia wanawake wanaofanya vizuri kwenye muziki duniani, lazima Rihanna atakuwa kwenye orodha hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa katika fani hiyo yenye mashabiki wengi kila kona ya ulimwengu.
Licha ya uwezo wake mkubwa alionao katika uimbaji ni miongoni mwa wanamuziki wa kike, wenye muonekano na haiba ya aina yake.
Uzuri wa sura na umbo lake unamfanya kuwa mwanamke ambaye anavutia kutazamwa na watu wa jinsia zote, hasa wembamba na urefu wake mithili ya twiga.
Kama walivyo warembo wake, mwanamuziki huyu hutumia umbile lake hilo kuvaa nguo za mitindo ya kila aina ambayo mingi kati ya hiyo humfanya kuvutia zaidi.
Mvuto huo ulimfanya kupewa sifa ya ubalozi wa mitindo na kuwa miongoni mwa wasanii ambao wanasifika kwa kwenda na wakati hasa katika sekta nzima ya mitindo.
Huenda sifa hiyo ndiyo imemfanya hivi karibuni kuzua gumzo katika maeneo mbalimbali kutokana na aina ya nguo ambazo mwanadada huyu hutoka nazo hadharani huku akitambua fika kuwa zinaacha wazi sehemu kubwa ya mwili wake.
Zaidi ya mara tatu Rihhana ameonekana akiwa katika mavazi ya ajabu, ambayo mwisho wa siku hupelekea kuibuka kwa majadiliano katika mitandao ya kijamii.
Kana kwamba hiyo haitoshi ilifika wakati mtandao wa Instagram ulilazimika kuifunga akaunti ya mwanamuziki huyo kutokana na kuweka picha ambazo zinamuonyesha akiwa na mavazi yasiyostahili.
Ingawa kujadiliwa kwa mtindo huu kunachangia kuzidi kumuongezea umaarufu nyota huyu, lakini kwa upande mwingine amekuwa akiwachukiza baadhi ya mashabiki wake ambao wanaonekana wazi kukerwa na mwenendo huo.
Pamoja na hitilafu hiyo katika mavazi Rihanna bado ni miongoni mwa wasichana wanaofanya vizuri kwenye ‘game’ mpaka hivi sasa.
Nyota ya mwanadada huyu asiyeishiwa na vituko ilianza kung’ara mwaka 2005, alipotoa nyimbo kadhaa zikiwemo Music on the Sun, A girl like me.
Uwezo wa hali ya juu wa nyota huyu ulionekana mwaka 2006 alipoachia wimbo wa Pon de Replay ambao ulionekana kubamba katika chati cha muziki ulimwenguni kote.
Diamonds, Disturbia, Te Amo, Rehab, Unfaithfully, Only girl ni miongoni mwa kazi zake ambazo zimefanya vizuri na kumwezesha kutunikiwa tuzo tatu za Grammy mpaka sasa ukiachilia mbali tuzo nyingine kadhaa ambazo anazo mwanadada huyu.
Rihanna kwa sasa yuko kwenye maandalizi ya kuachia albamu yake ya nane baada ya saba za awali kufanya vizuri kwenye mauzo, kiasi cha kuweka rekodi ya kuwa mwanamuziki anayefanya vizuri sokoni.
Miongoni mwa albamu ambazo zilishatoka ni pamoja na Music on the Sun, A girl like me, Good girl gone bad, Rated R, Loud, Talk that Talk na Unapologetic.
Imeandaliwa na Elizabeth Edward kwa msaada wa mashirika ya habari

Post a Comment

 
Top