New York, Marekani. Tanzania imesisitiza kuwa
ushirikiano wa kimaendeleo ni eneo muhimu katika kupunguza umaskini na
katika kuzijengea uwezo na mazingira ambayo hatimaye yataziwezesha nchi
zinazoendelea kupunguza utegemezi.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu
Nchemba kwenye mjadala kuhusu hatua za kimataifa kuelekea 2015 na mifumo
ya ufuatiliaji na uwajibikaji kwa ushirikiano wa kimaendeleo.
Nchemba ambaye alikuwa mmoja wa wanajopo wanne
walioongoza mjadala huo uliohusisha mawaziri, wabunge, wasomi, wafafiti
na wajumbe kutoka Taasisi zisizo za kiserikali duniani, alisema
uanzishwaji mpya wa ushirikiano wa maendeleo baada ya mwaka 2015,
unatakiwa kuendelezwa kama ulivyoainishwa katika lengo la nane la
Malengo ya Milenia (MDGs).
Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka
miwili umefanyika chini ya mwamvuli wa Baraza la Umoja wa Mataifa
linalohusika na Masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii (ECOSOC).
Akitilia mkazo kuhusu eneo hilo la ushirikiano wa
kimaendeleo, Naibu Waziri alisema ushirikiano huo lazima pia ujengeke
katika mazingira ya kuaminiana, kuwajibika na kuwa na mifumo ya
ufuatiliaji.
Akizungumzia kuhusu misaada ya maendeleo (ODA),
kuwa ingawa misaada hiyo ya maendeleo bado ni muhimu hususan kwa nchi
zinazoendelea, lakini mchango wake si mkubwa sana katika eneo la
maendeleo kwa ujumla wake. Nchemba aliyataja maeneo ambayo yanaweza
kuzalisha mapato mapya ya ndani kuwa ni pamoja na ukusanyaji wa kodi na
udhibiti wa fedha chafu.
“Uimarishaji wa vyanzo hivyo vya mapato, udhibiti
wake, uwajibikaji pamoja na ushirikiano wa kimaendeleo, ndipo mataifa
yanayoendelea yataweza kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje,”
alisisitiza Nchemba.
Post a Comment