Karagwe. Vitendo vya ukatili na unyanyasaji
dhidi ya watoto wenye ulemavu wilayani Karagwe, vimezidi kukithiri huku
wadau wanaotetea haki za watoto wakiendelea kutoa wito kwa wananchi
kutoa ushirikiano kukabiliana na tatizo hilo.
Hayo yalibainika juzi baada wadau wanaotetea haki
za watoto kumtembelea Apewe Mathayo (12), ambaye ni mtoto mwenye ulemavu
wa viungo aliyefungiwa ndani kwa miaka 11.
Mtoto huyo aliokolewa na mkazi wa Kijiji cha Kamagambo, Kata ya Kiruruma, wilayani Karagwe, baada ya kutelekezwa na wazazi wake.
Shirika la kuhudumia walemavu la Karagwe Community
Based Rehabilitation Programme (KCBRP) kwa kushirikiana na wadau
wanaotetea haki za mtoto ambao ni Dawati la Jinsia la Polisi Karagwe,
Ofisa Ustawi wa Jamii na viongozi ngazi ya kijiji walikwenda nyumbani
kwa Mathayo Rwakibala kufuatilia maendeleo ya mtoto huyo.
Apewe anadaiwa kutelekezwa na wazazi wake kwa
miaka 11 kwa kufungiwa ndani hadi Septemba mwaka jana alipogunduliwa na
Biashara Severian, ambaye alitoa taarifa kwa Shirika la KCBRP ambalo
lilianza kumhudumia.
Katibu Mtendaji wa KCBRP, Aggrey Mashanda alisema
tangu kutambuliwa kwa mtoto huyo wamepeleka msaada wa vitu mbalimbali
vikiwamo mavazi, vyakula vya lishe, kukarabati chumba anacholala,
kununua godoro na kitanda.
Misaada mingine ni kumnunulia ng’ombe wa maziwa, lakini jitihada zote hazijazaa matunda kutokana na familia hiyo kutomjali.
Mashanda alisema wameshirikisha wazazi wake
kuchangia kiwango kidogo ili waanzishiwe mradi wa kuingiza kipato,
lakini familia hiyo haijaonyesha ushirikiano na imeshindwa kumpeleka
Hospitali ya Kagondo kufanya mazoezi.
Baba ya mzazi wa mtoto huyo, Rwakibala aliahidi
kutimiza ushauri wote aliopewa na wadau hao, huku akikiri kuwa yupo
tayari kutoa huduma zinazostahili kwa mtoto huyo na kuacha kumnyanyasa
mke wake.
Naye Ofisa Ustawi Jamii Wilaya ya Karagwe,
Owokusima Kaihura aliagiza familia hiyo kuhakikisha inampa mtoto huyo
matunzo na huduma stahili na kwamba, bila kufanya hivyo sheria itachukua
mkondo wake.
Post a Comment