Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.PICHA|MAKTABA
Dodoma. Waziri ya Fedha, Saada Salum Mkuya jana
aliwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2014, ambao umefuta
misamaha ya kodi katika maeneo yaliyokuwa yakilalamikiwa na watu wa kada
mbalimbali nchini.
Katika muswada huo Serikali imefuta misamaha ya
kodi ya mapato inayotokana na michezo kubahatisha na ukodishaji wa
ndege nje ya nchi.
“Muswada umependekeza waziri husika kutotoa
msamaha wa ushuru wa mafuta kwenye mafuta isipokuwa mafuta ya petroli
yanayotumika kwenye miradi mbalimbali inayofadhiliwa na washirika wa
maendeleo,” alisema Mkuya.
Mkuya alisema kuwa katika muswada huo, Serikali
imeondoa saruji, nondo na mabati katika orodha ya bidhaa zinazochukuliwa
kuwa ni bidhaa za mtaji ambazo kwa sasa hupata msamaha wa kodi kupitia
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
“Lengo ni kuhamasisha uzalishaji wa saruji, nondo
na mabati pamoja na kulinda viwanda vya uzalishaji wa bidhaa hizo hapa
nchini dhidi ya ushindani wa bidhaa za aina hiyo zinazoingizwa nchini
kutoka nje ya nchi,”alisema Mkuya.
Alisema kuwa Serikali imefuta msamaha wa kodi ya
mapato yanayotokana na ukodishaji wa ndege nje ya nchi ili kupunguza
misamaha isiyokuwa na tija.
“Marekebisho haya yanalenga kutoza mapato
yanayotokana na ukodishaji wa ndege nje ya nchi, badala ya kusamehe kodi
ya mlipakodi asiye mkazi, ambaye hatimaye hulazimika kulipa kodi
itokanayo na mapato hayo nchini kwake,”alisema Mkuya.
Marekebisho hayo yanapendekeza kufuta misamaha ya
kodi inayotolewa kwa kampuni ya simu isipokuwa vifaa vya ujenzi wa
minara ya simu.
Pamoja na marekebisho hayo muswada huo
unapendekeza kuongeza kifungu cha 3(d) ili mtu yoyote asiruhusiwe kutoa
misamaha ya kodi kwa miradi nayohusu upanuzi na ukarabati wa miradi
inayofanywa na wawekezaji.
Aidha ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji baridi
(soda) pamoja na kwenye maji ya matunda (juice), iliyotengezwa kwa
matunda yanayozalishwa hapa nchini utabaki kama ulivyo sasa ili
kuimarisha viwanda vya ndani.
Mkuya alisema vinywaji baridi vimefanyiwa
marekebisho ambapo ushuru kwenye vinywaji hivyo utapunguzwa kutoka Sh 91
kwa lita hadi Sh 55 kwa lita.
Post a Comment