Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano), Samia Suluhu Hassan alikataa kueleza walipo waasisi sita wa
Muungano ambao kambi ya upinzani ilidai kuwa waliuawa na kuzikwa
handaki moja, badala yake akatumia nafasi hiyo kumshambulia mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu akidai hizo ni propaganda na upotoshaji.
Juzi wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani, Lissu aliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za
kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa Tangayika na Zanzibar na kuzikwa
katika handaki moja visiwani Zanzibar.
Lissu aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdalah Kassim
Hanga, aliyekuwa waziri mkuu, Abdul Aziz Twalam aliyekuwa Waziri wa
Fedha na Abdulaziz na Saleh Akida aliyekuwa mjumbe wa Baraza la
Mapinduzi Zanzibar.
Pia aliwataja Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha
Ubwa ambao alisema nao waliuawa na kuzikwa katika handaki moja eneo la
Kama nje kidogo ya Zanzibar.
“Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa,
walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo...
tunataka kuambiwa ukweli kwanini mchango wao kuhusu Muungano umefichwa,”
alisema Lissu juzi.
Lakini alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri
Hassan alionekana kuzigeuza hoja hizo kuwa ni za Lissu pekee badala ya
kambi ya upinzani na kumshambulia mbunge huyo akidai kuwa ni mpotoshaji,
anayepiga propaganda na mchochezi.
Waziri huyo, ambaye ni Mzanzibari, alisema
alipuuza maswali yote kuhusu waasisi hao akisema mbunge huyo wa Chadema
alipotoka katika hotuba yake na ndio maana hakutaka kuzungumzia katika
majumuisho ya bajeti ya ofisi yake bungeni.
“Yule Lissu sio mkweli na ndio maana sisi tulimpuuza,” alisema waziri huyo.
“Hakuna kitu kama hicho na endapo kingekuwepo sisi
Serikali tungeshatoa ufafanuzi ili watu wapate kujua ukweli wake,”
aliongeza Waziri Samia bila kutoa ufafanuzi wa nini kiliwatokea watu hao
walioshika nafasi za juu serikalini mara baada ya Mapinduzi na Muungano
wa Zanzibar na Tanganyika.
Pamoja na kudai kuwa aliona hoja hizo ni
upotoshaji, Waziri huyo, ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Bunge la
Katiba, aliwasihi wabunge wa upinzani kupeleka hoja zao katika Bunge
Maalumu la Katiba linalojadili uundwaji wa Katiba Mpya, ambalo pia
limetawaliwa na suala la muundo wa Muungano na kero zake.
Waziri Samia alisema hoja hizo zinalenga
kuwaaminisha Watanzania mambo ambayo hayapo ili kuwajaza chuki dhidi ya
Serikali yao na pia alidai zina uchochezi ndani yake.
Waziri Samia aliwashauri wabunge pamoja na
Watanzania kupuuza kauli hizo akidai mbunge huyo hautakii mema Muungano
na ndio maana anaibua mambo aliyodai kuwa ni ya uongo na ya uchochezi.
Madai ya Lissu
Lissu alitoa madai hayo akinukuu kitabu cha
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru kilichoandikwa na Harith Ghassany ambacho
kinaonyesha jinsi ambavyo viongozi hao wa SMZ waliuawa na kuzikwa
katika kaburi moja.
“Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli
juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na
kuzikwa katika kaburi au handaki moja,” alisema Lissu.
Jitihada za kumpata Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ,
Balozi Seif Ali Idd na Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Mohamed Abood
kuzungumzia msimamo wa SMZ kuhusu kauli hiyo hazikuzaa matunda kwa kuwa
simu zao ziliita bila majibu.
Akizungumzia suala hilo, mbunge wa viti maalumu,
Anna Abdallah alisema naye alidai hoja hizo za Lissu ni za uchochezi
ambao usipopuuzwa, unaweza kusababisha chuki kwa jamii.
“Ule ulikuwa ni uchochezi, na upinzani wa aina
hiyo ni wa ajabu sana… kwa mtazamo wake yeye anafikiri anawafurahisha
Wazanzibari, lakini wamemuona ni mtu wa ajabu,” alisema mwanasiasa huyo
mkongwe.
Pamoja na uzito wa tuhuma hizo, baadhi ya wabunge
waliohojiwa na gazeti hili jana walionekana kuzungumza kimkakati kwamba
hawakusikiliza hotuba hiyo.
Utata mkubwa bado umezunguka kutoweka kwa Hanga na
wenzake machapisho mbalimbali yanawatambua kama watu waliokuwa mstari
wa mbele katika Mapinduzi ya Zanzibar na ambao waliunga mkono Muungano
mara baada ya mapinduzi hayo.
Post a Comment