Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP), Hellen Clark akikabidhi moja ya kompyuta mpakato kati ya 60 kwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damiani Luvuva, alipokutana na wakuu wa NEC, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) pamoja na mabalozi wa nchi mbali mbali za Ulaya, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka NEC, Julius Malaba. Picha na Emmanuel Herman
Dar es Salaam. Shirika la Mpango wa Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP) limeeleza nia ya kuisaidia Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) ili ifanikishe matumizi ya mashine za kisasa za Biometric
Voters Register (BVR) wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Hellen Clark alitoa
ahadi hiyo jana na kuongeza kuwa hata hivyo, matumizi ya mashine hizo
yamechelewa kwani zilitakiwa zitumike tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,
muda uliobaki unahitaji utekelezaji ili zitumike mwakani.
Clark ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani wa New
Zealand, alisema hayo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ziara yake
ya siku nne nchini.
Alisema alipokuja nchini mwaka 2010 alitembelea
NEC na kuziona kompyuta zilizokuwa zikitumika kusajili wapigakura kuwa
zilikuwa zinatumia mfumo uliopitwa na wakati.
“Natambua kuwa kuna mpango wa kuwenda kwenye
mashine za BVR ambazo zitahusisha uchukuaji wa alama za vidole na mambo
mengine, natambua kuwa uamuzi umeshachukuliwa kuhusu mfumo huo,
umechelewa, lakini sasa utekelezaji unatakiwa,” alisema.
Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda kulitaarifu Bunge mjini Dodoma kuwa NEC inaendelea
na maandalizi ya kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha
daftari la kudumu la wapigakura.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akisoma
hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya
matumizi ya fedha ya ofisi yake na ofisi ya bunge kwa mwaka 2014/15.
Katika hotuba yake, Pinda alieleza kuwa mfumo wa
BVR utakaotumika ni tofauti na mfumo wa awali wa Optical Mark
Recognition (OMR) ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu
Damian Lubuva akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema kuwa
mashine za BVR zitatumika wakati wa uandikishaji wapigakura pekee yake.
Akizungumza kwa kujiamini, Hellen alisema Tanzania imeshafanya uchaguzi mara nne kwa mafanikio makubwa.
Alisisitiza kuwa UNDP ipo tayari kutoa msaada
wowote wa kiufundi ingawa mpango huo ni wa kitaifa, lakini mradi wa wa
shirika hilo unatoa nafasi kuisaidia NEC.
Clark ambaye ameshafanya ziara nne nchini, alisema
kuwa wadau mbalimbali wanaoshirikiana na shirika lake wameshatoa dola
22 milioni sawa na Sh35.2 bilioni kusaidia mchakato wa uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwakani.
“Hali kadhalika, tutashirikiana nanyi katika kuhakikisha
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanashiriki kwenye uchaguzi huo,”
aliongeza.
Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe wakati akiwasilisha taarifa ya kambi yake bungeni
kwenye Bunge la bajeti mwaka jana, alimtaka Waziri Mkuu Pinda kuiamuru
NEC kusimamisha maandalizi ya mfumo wa uchaguzi wa elektroniki hadi hapo
itakapowashirikisha wadau.
Mbowe alisema tayari NEC imekiri kuanza maandalizi huku wadau wa uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa hawajashirikishwa.
Ujangili Tanzania
Akieleza masuala aliyozungumza na Rais Jakaya
Kikwete, Clark alisema kuwa alimwelezea changamoto za ujangili na
umaskini aliouona alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwamba kuna
umaskini mkubwa, njaa, watoto hawapati elimu ya kutosha na kinamama
wajawazito wanakufa kwa sababu zinazoweza kuzuilika.
Post a Comment