0
NIMSHUKURU Mungu kwa kuweza kunipa uhai leo na kunifanya niweze kuyaandika haya niliyoyakusudia.
Mada kuu kila kona hivi sasa hapa nchini ni muundo gani wa serikali utafaa kufuatwa na nchi yetu.
Hakika kitu kinachosumbua vichwa vya wengi siyo muundo wa serikali, bali ni aina gani ya muundo wa serikali unaoweza kuunusuru muungano huu uliodumu kwa miaka 50.
Wapo watu wanaotaka iwepo serikali moja japokuwa hili nina uhakika kwa asilimia mia moja kuwa ni ndoto za mchana kwani haiwezi kukubalika kwa Wazanzibari.
Wanasema waziwazi kuwa hawatakubali kupoteza utaifa wao ndiyo maana wana wimbo wao wa taifa, bendera yao, bunge lao na serikali yao!
Wapo pia wanaotaka serikali mbili ambao ni msimamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jambo ambalo halikubaliki kwa wale wanaohitaji kurejesha Serikali ya Tanganyika.
Wanasiasa wa Chadema chini ya uongozi wa Freeman Mbowe, CUF ambacho mwenyekiti wake ni Profesa Ibrahimu Lipumba na NCCR Mageuzi chini ya James Mbatia pamoja na DP kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila.
‘Waumini’ hao wa serikali tatu wanaambiwa kuwa wanahatarisha muungano na wanaosema ni wale walio madarakani.
Tujikumbushe miaka ya nyuma ni kwamba hofu kuhusu muungano uliopo kusambaratishwa kupitia muundo huo wa serikali tatu, zilianza kujitokeza tangu mwaka 1984  baada ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi kuidhinisha mapendekezo ya Zanzibar kutaka mamlaka kamili.
Madai hayo ya Alhaji Jumbe yalimkasirisha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyemtaka Aboud Jumbe ajiuzulu nafasi zake zote tatu za uongozi.
Baadhi ya Wazanzibari walichukizwa mno na kitendo hicho na kutoa madai kuwa nchi yao inatawaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina koti la Tangayika.
Walihoji iweje rais wao waliyemchagua kidemokrasia aondolewe madarakani bila wao ama serikali yao kuhusishwa?
Uamuzi huo, pamoja na pingamizi mbalimbali zilizojitokeza kupitia mapendekezo ya tume kama vile ya Jaji Nyalali na Tume ya Jaji Kisanga zilizoundwa baadaye na hata kundi la Wabunge 55 yaani G55 kujaribu kuja na hoja ya muundo wa serikali tatu, zimeonekana kwa wengine hasa watawala kuwa zitahatarisha muungano.
Baadhi ya kauli za viongozi, akiwamo Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika siku za karibuni zimeonesha misimamo kuwa serikali mbili ndiyo jawabu.
Hivi karibuni serikali, wasomi, viongozi wa kitaifa walioshiriki maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano wameonekana kuhubiri kwamba nchi yetu iendelee kuwa na serikali mbili na kwamba tatu zitavunja muungano.
Hata hivyo, msimamo huo unakinzana na ule wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaosema kuwa mtazamo wa viongozi wa CCM, hatima ya muungano ni chama hiki kubakia madarakani milele badala ya kuona serikali tatu zikipatikana.
Kutokana na historia ya kukataliwa kwa maoni ya muundo wa serikali tatu, pengine ni lazima CCM itawale milele ili kunusuru muundo wake wa serikali mbili.
Lakini, hatutaki kufikia huko, tunataka kila chama kitakachoingia madarakani kiheshimu Katiba ya Tanzania ambayo ndiyo sheria mama.
Ninaamini muda umefika wa maridhiano kati ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu muundo wa serikali na hili linajadilika.
Atakayepinga maridhiano ni adui wa taifa letu.

Post a Comment

 
Top