0

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh  

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atatumia siku 45 kuchunguza kashfa ya ufisadi wa zaidi ya Sh200 bilioni zilizolipwa kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kutoka katika Akaunti ya Escrow.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana, zinasema CAG amemwandikia barua Katibu wa Bunge, akimwomba athibitishe rasimu ya hadidu za rejea 13 ambazo zitamwongoza katika ukaguzi huo unaosubiriwa na Bunge, wanasiasa na wananchi.
Moja ya hadidu za rejea ni uchunguzi wa iwapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) aliisamehe kampuni hiyo kodi inayofikia Sh26 bilioni.
Mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilieleza Bunge kuwa ukaguzi katika akaunti hiyo ungefanywa na Ofisi ya CAG na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Sakata la hilo la IPTL liliibuliwa na Gazeti dada la The Citizen na Mwananchi, baadaye Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), akalipua bungeni ufisadi katika Akaunti hiyo ya Escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wiki iliyopita, Kafulila aliliomba Bunge liunde kamati teule kuchunguza ufisadi huo akisema ni mkubwa kuliko ule Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ambayo pia ilikuwa ya BoT.
Hoja yake iliungwa mkono na wabunge kadhaa akiwamo, John Mnyika (Chadema - Ubungo), ambaye alipinga Takukuru kuchunguza akisema ndiyo iliyoisafisha Serikali katika kashfa ya Richmond.
Hata hivyo, baada ya mvutano mkali, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitumia mamlaka yake kukubaliana na pendekezo la Waziri Mkuu la kutaka CAG na Takukuru wachunguze.
AG Frederick Werema alipopigiwa simu jana kuhusu suala hilo alisema: “Nimepumzika, sina muda wa kujibu maswali yako.”
Barua ya CAG
“Pamoja na barua hii, ninaleta rasimu ya hadidu za rejea zilizounganishwa na zile zilizotoka kwa Katibu Mkuu Nishati kwa ajili ya kuridhiwa na ofisi yako kabla ya ukaguzi maalumu kuanza,” inasomeka sehemu ya barua hiyo ambao CAG Ludovick Utouh alikiri kuiandika akisema: “Ni kweli nimewatumia hizo hadidu za rejea.”
Kuhusu muda wa uchunguzi, Utouh alisema: “Hizo siku 45 ni makadirio tu lakini tutafanya kwa sababu tunajua kuna shinikizo kubwa linahusika ila itategemeana pia na ugumu wa kazi tutakayokutana nayo.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa jana alisema ingawa hajaiona, amesikia kuwapo kwa barua hiyo katika Ofisi ya Katibu wa Bunge.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah ambaye ofisi yake ilipokea barua hiyo Aprili 23, mwaka huu, hakupatikana jana.
Maeneo yatakayozingatiwa katika ukaguzi huo yametajwa kuwa ni pamoja na CAG kuchunguza utekelezaji wa mkataba wa kuzalisha umeme kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Kuchunguza iwapo BoT ilitimiza wajibu wake na kuchukua tahadhari ya kutosha kabla ya kuhamisha Dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh8, 020,522,330.37.
Pia, CAG ametakiwa kuchunguza iwapo BoT ilitimiza wajibu wake na kuchukua tahadhari wakati wa kuhamisha hati fungani zenye thamani ya Sh153.36 bilioni kutoka Escrow kwenda IPTL.
Katika hadidu hizo za rejea, CAG anatakiwa kuchunguza sababu za kufunguliwa kwa Akaunti ya Escrow pia chanzo cha mgogoro kuhusu tozo kati ya Tanesco na IPTL.
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo gazeti hili limeiona, CAG atachunguza iwapo wakati akaunti hiyo inafunguliwa, Kampuni ya Mechmar ilikuwa ina hisa za umiliki katika Kampuni ya IPTL.
“Pia kuthibitisha kama Mechmar ilikuwa imehamisha umiliki wake kwenda Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP) kabla ya kufilisiwa,” inasomeka moja ya hadidu za rejea.
Kulingana na hadidu hizo za rejea, CAG pia anatakiwa kuchunguza kiwango cha fedha kilichopaswa kuwapo kwenye Akaunti ya Escrow wakati BoT inahamisha fedha kwenda IPTL.
Kazi hiyo ya CAG itahusisha pia kuchunguza na kutoa taarifa kuhusu kiasi cha fedha kilichowekwa na kila mhusika hadi uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kesi ulipotolewa.
“Kuchunguza madai ya Benki ya Standard Chartered (Hongkong) kwa IPTL na madai mengine ya kuzalisha umeme wa IPTL na kama Serikali imejihadhari na uwezekano wa madai yanayoweza kufunguliwa dhidi yake na wadai mbalimbali,” inasomeka barua hiyo ikiomba Bunge lithibitishe hadidu hizo kabla ya kuanza ukaguzi.
Pia CAG atachunguza iwapo Wizara ya Nishati na Madini ambayo iliingia mkataba na IPTL kufungua akaunti hiyo ilifanya uadilifu na kuweka uangalifu kabla ya kutoa fedha zilizokuwapo kwenye akaunti.
CAG amegizwa pia kufanya uchunguzi kuhusu hisa za Mechmar inayosemekana kufilisika na iliyokuwa na hisa nyingi IPTL na kama hisa hizo sasa zinamilikiwa na PAP na ametakiwa kutoa mapendekezo ya njia sahihi za kisheria zinazoweza kutumika kwa ajili ya kulinda Serikali isipate hasara katika utekelezaji mkataba wa IPTL.
Ukaguzi huo utahusisha pia shughuli zote (transaction) zilizofanyika kuhusiana na suala hilo kuanzia Julai Mosi, 2006 hadi Machi 31, mwaka huu na wakaguzi wameruhusiwa kuongezea mawanda.

Post a Comment

 
Top