Mbeya. Wafanyabishara wa matunda aina ya maparachichi katika
Soko la Wakulima la Soweto Mkoa wa Mbeya, wameiomba Serikali na wadau
mbalimbali kutoa miche ya kisasa kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa
wingi na kuboresha maisha yao.
Wamesema ubora wa maparachichi yanayozalishwa
mkoani Mbeya sasa yameanza kuzidiwa na yale ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa
kuwa wanatumia miche bora.
Mfanyabiashara Athanas Saimon akiwa kwenye soko
hilo alisema maparachichi yanayopatikana wilayani Rungwe mkoani Mbeya
yameshuka ubora kutokana na kutumia miti ya asili wakati mkoani
Kilimanjaro wanatumia miche ya kisasa.
Alisema kwa kuzingatia ubora, gunia moja la
maparachichi kutoka Kilimanjaro kwa sasa linauzwa Sh100,000 wakati ya
kutoka Rungwe yakiuzwa kwa bei pungufu ya hiyo.
“Tunataka Serikali itusaidie kupata miche bora ili
wakulima waipande na kuzalisha matunda mengi ya kuweza kusindika kwenye
kiwanda kilichopo Rungwe’’ alisema.
Aidha baadhi ya wakulima waliomba kupatiwa mikopo
isiyokuwa na riba ili kuwawezesha kubuni miradi endelevu licha ya
kutegemea kilimo ambapo kwa sasa mazao mengi yameingia katika ushindani
wa masoko na hivyo kupelekea baadhi ya wakulima kutonufaika na kilimo na
badala yake wafanyabishara wamekuwa wakiingia mashambani kuwarubuni
wakulima.
Post a Comment