0

Kigoma. Shura ya Maimamu Mkoa wa Kigoma wametoa maazimio yao kutokana na sakata la kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda ambapo amekataliwa kupewa dhamana, jambo wanalodai ni kinyume cha sheria za nchi kwa vile kosa lake lipo wazi kupewa dhamana.
Katika maazimio yao wamekubaliana kufanya kampeni za kuing’oa CCM madarakani kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji, mitaa, kata, majimbo hadi Taifa katika chaguzi mbalimbali endapo Serikali itakataa kuunda tume huru ya kuchunguza sakata zima la Sheikh Ponda kushambuliwa kwa risasi alipokuwa katika mkutano wa Waislamu mjini Morogoro Agosti 18 mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano ulioshirikisha Waislamu kutoka Wilaya ya Kigoma, Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu Mkoa wa Kigoma, Sheikh Ibrahim Ramadhan alisema kamwe hawatakubaliana na taarifa yoyote itakayotolewa na Polisi kwa sababu wamepoteza imani na jeshi hilo.
Pia alilaani kauli iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kwamba polisi wapo tayari kupambana na yeyote atakayeonekana kuandamana kutaka Ponda aachiwe.
Alilaumu kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyotoa bungeni kuwataka Polisi kupiga wananchi kwa kisingizio cha kutotii sheria kuwa ndizo zinazosababisha viongozi wa dini kupigwa na polisi mara kwa mara kwa kupata vipigo bila sababu za msingi.

Post a Comment

 
Top