Arusha. Jaji Mkuu nchini, Mohamed Chande Othman, amevitaka
vyombo vya dola, viongozi na wananchi kufanya kazi kwa kuheshimu Katiba
na Utawala wa Sheria badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Akizungumzia suala la utii wa sheria nchini, mara
baada ya kufungua kongamano la kwanza la majaji wanawake barani Afrika,
alisema kila mtu yupo sawa mbele ya sheria.
“Lazima ieleweke nchi hii inaongozwa kwa kufuata
misingi ya sheria, hairuhusiwi mtu yeyote kutumia mamlaka yake kukiuka
sheria kwani kila mtu lazima aheshimiwe , haki haitegemei uzito wa mtu
au pesa ya mtu” alisema Jaji Chande.
Alisema Serikali inapaswa kuheshimu sheria, polisi
wanapaswa kuheshimu sheria na pia raia wanawapaswa kuheshimu sheria
hata kama zina upungufu.
“Kama sheria ina upungufu inafaa kupelekwa bungeni katika chombo cha kutunga sheria na sio kuvunja sheria,” alisema Jaji Chande.
Alisema katika kufuata misingi ya sheria na utawala bora kila chombo katika jamii kina nafasi yake.
“Polisi kazi yao ni kuchunguza, Idara ya Mwendesha Mashtaka ni kushtaki na Mahakama ni kutoa hukumu “alisema Jaji Chande.
Alisema ni lazima mwamko wa kuheshimu sheria uwepo
na kuepuka watu kujichukulia sheria mikononi kama kujiita watu wenye
hasira kali.
“Kila mtu anapaswa kuheshimu na kutii sheria na hakuna ambaye yupo juu ya sheria”alisema Jaji Chande.
Kauli ya Jaji Chande imekuja siku moja baada ya
kuibuka sakata la kushambuliwa kwa kinachodaiwa ni risasi, Katibu wa
Taasisi ya Kutetea Haki za Waislam nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Tukio hilo la aina yake, lililotokea mkoani Morogoro, wakati Sheikh
Ponda akiwa anaelekea kuswali katika msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja,
baada ya kumalizika mhadhara katika Kiwanja cha Shule ya Msingi Uwanja
wa Ndege.
Sheikh Ponda alilazwa hospitali ya Taifa Muhimbili
kwa matibabu , lakini Serikali imepewa jukumu la kuhakikisha inafanya
kazi ya ziada kutoa maelezo yaliyo sahihi juu ya tukio hilo.
Polisi wametangaza kuunda tume kuchunguza tukio hilo na wameahidi kushirikiana na vyombo vingine. . dola.
Post a Comment