WATOTO 11 kutoka familia tofauti wamekamatwa mjini Singida, wakidaiwa
kufanya vitendo vya ngono kwenye nyumba moja usiku wa kuamkia juzi.
Kikundi cha ulinzi shirikishi jamii, ndicho kilikamata watoto hao,
wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 16, wa kike na kiume,
wakiwa ndani ya chumba kimoja.
Inadaiwa kundi hilo la watoto, limeacha shule na kukimbia kwa wazazi
wao, kisha kujiingiza kwenye vitendo vya mapenzi katika umri mdogo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mwenyekiti wa
Mtaa wa Bima, Salum Sudi alisema alipokea taarifa kuhusu watoto hao
kutoka kwa mwenye nyumba walikokutwa.
Kwa mujibu wa Sudi, mwanamke huyo mmiliki anaishi jirani na nyumba
hiyo, ambayo hutumiwa na mmoja wa watoto wake wa kiume kulala.
Mwenyekiti wa Mtaa alimkariri mama huyo, akisema alishtuka kutoka
usingizini, kutokana na kelele za watoto hao usiku wa manane na akaenda
kuita kikundi cha ulinzi shirikishi baada ya kujionea vitendo vichafu,
vilivyokuwa vinafanyika.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mtunduruni, Petronila Katundu walikopelekwa
watoto hao kwa ajili ya mahojiano zaidi, alisema hana cha kufanya,
zaidi ya kuwaachia polisi wawachukulie hatua wazazi na walezi wa watoto
hao.
Hata hivyo, wazazi na ndugu waliokuwepo eneo la tukio, walisema
baadhi ya watoto hao wameshindikana na wameacha shule, kisha kuamua
kujihusisha na vitendo vya mapenzi katika umri mdogo.
Tukio hili la baadhi ya watoto kuacha shule na kujihusisha na vitendo
vya ngono katika umri mdogo, limekuja huku takwimu za mkoa zikionesha
kuwa zaidi ya watoto 20,000 wanaishi katika mazingira hatarishi mkoani
Singida.
Post a Comment