0
Kuna semi maarufu za wahenga kuwa, ‘Usipoziba ufa utajenga ukuta’ na ‘Heri ya nusu shari kuliko shari kamili’.
Semi hizi na nyinginezo zimekuwa zikitolewa kwa lengo la kutoa hadhari kuwa ni muhimu kuchukua hadhari kabla ya kupatwa na janga.
Tunaambiwa kuwa usipoziba ufa utajenga ukuta tukipewa angalizo kuwa tusipozuia tatizo kabla halijawa kubwa, kwkazi ya kulitatua itakuwa ngumu kwa kusubiri hadi liwe kubwa, kiasi kwamba litashindikana kabisa kutatuliwa.
Katika jamii yetu tuna biashara ambazo zimekuwa zikifanywa zikiwamo za kuuza fedha au chenji ambazo zinaonekana kwa wingi katika mitaa yetu ikiwamo kwenye vituo vya mabasi.
Biashara hii siyo ngeni machoni mwa watu wengi kwani karibu kwenye kila kituo cha basi jijini Dar es Salaam inafanyika.
Biashara hii hufanyika baina ya makondakta wa daladala na wauza chenji kwa kutoa noti na kupewa sarafu.
Kwa kiasi fulani, biashara hii nayo ni moja ya zile zilizopunguza uhaba wa ajira kwa vijana baada ya vijana kujiajiri bila kujali ni wa umri au kabila gani, ingawa wengi wanaofanya biashara hiyo ni vijana ambao wako tayari kukimbizana na magari katika baadhi ya maeneo.
Katika baadhi ya maeneo biashara hii inafanywa na watu wa rika zote kwa kuwa hukaa na fedha ambazo wamezipanga kwenye meza na wateja wakija hununua tena kwa utulivu.
Ni biashara ambayo imetoa ajira, imepunguza adha, ugomvi baina ya makondakta na abiria wao, imepunguza hata uhalifu kwa kuwa vijana wengine ambao wangefanya mambo hayo sasa wamepata kazi ya kufanya vizuri zaidi kwani wamejiajiri.
Hata hivyo, wasiwasi wangu ni kuhusu vijana wanaofanya biashara hiyo kutokujua madhara kwa afya na kutokufahamu athari zake.
Wataalamu wa afya na tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa fedha hasa sarafu zina madhara kwa afya ya binadamu kutokana na mzunguko wake ulivyo mkubwa.
Kwa mfano, tunaambiwa kuwa fedha inatembea kuliko pengine anavyotembea mtumiaji wake.
Haichagui wa kuitumia, wanaitumia wenye akili timamu na hata wasiokuwa nazo, hivyo inategemea mtu wa mwisho aliitumia vipi kwa kuwa kuna watu wanajifutia jasho noti bila kujali kuwa atampa mtu mwingine.
Kuna baadhi ya watu wanahifadhi fedha hizo zikiwamo sarafu na noti kwenye sehemu zisizo salama.
Tunaambiwa fedha zina madhara, wakati mwingine zinaweza kusababisha maradhi kwa kuwa zinabeba vimelea vya magonjwa kwa urahisi kutokana na kuwa katika mzunguko siku zote.
Uchunguzi umebaini kuwa fedha za noti na zile za sarafu huweza kukusanya na kusambaza vimelea vya magonjwa hatari kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Vimelea hivyo vina uwezo wa kusababisha maradhi kama ya ngozi, kuharisha, magonjwa ya fizi, homa za vipindi na mengineyo. Kibaya zaidi magonjwa mengi huchukua muda hadi kujitokeza na yanapojitokeza huwa tayari yameshaleta madhara ambayo yameingia mwilini taratibu bila mhusika kujua.
Pamoja na kubeba vimelea hivyo, lakini fedha pia inao uwezo wa kubeba sumu kutoka eneo moja kupeleka lingine kulingana na mzunguko wake.
Kwa hiyo, ushauri wangu kwa wauza chenji na wateja wao ambao kazi yao kubwa ni kushika fedha baadhi wamekuwa wakijisahau na kula huku wakiwa nazo mkononi. Wanashauriwa waache tabia hiyo.

Post a Comment

 
Top