Rais Jakaya Kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na maaskofu wa kanisa la Katoliki mara baada ya kumalizika kwa ibada ya kumweka wakfu askofu mpya wa jimbo katoliki Shinyanga, Mhashamau baba Askofu Leberatus Sangu
Shinyanga. Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini
kutowaonea haya viongozi wa kisiasa wanaotaka kugeuza nyumba za ibada
kuwa majukwaa ya kufanyia siasa kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha
vita ya kidini au waumini kwa waumini.
Rais Kikwete alisema hayo jana wakati wa ibada ya
kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi, askofu mpya wa Jimbo la Shinyanga,
Liberatus Sangu katika Kanisa la Mama Mwenye Huruma, Parokia ya Ngokolo,
Shinyanga.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha makanisa na
misikiti inabaki kuwa sehemu ya ibada na usuluhishi na iwapo
watashindwa, inaweza kusababisha makundi na mapigano.
“Katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu,
wanasiasa wengi wanapenda kutumia tofauti za rangi, ukabila na dini
nawaomba msiruhusu mambo hayo ni hatari kwa Taifa, endeleeni kukemea
jambo lolote ambalo mnaona linakwenda tofauti.”
Rais Kikwete pia alizungumzia mauaji ya vikongwe
na albino huku alimtaka Askofu Sangu na maaskofu wengine kuongeza bidii
kuwalea waumini wao katika imani, ili waachane na vitendo vya
kishirikina ambavyo ndivyo chanzo cha mauaji yao.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Muadhama Polycarp Kardinali Pengo alimsimika rasmi Askofu Sangu na
kumkabidhi fimbo ya kichungaji huku akimtaka kuhakikisha anafanya kazi
kwa kushirikiana na viongozi wengine na kumtakia heri na baraka katika
muda wake wote wa kitume.
Kwa upande wake, Askofu Sangu alisema kazi kubwa
iliyo mbele yake ni kuhakikisha analinda na kustawisha mema yote
yaliyoachwa na waliomtangulia.
“Nitashirikiana na viongozi wenzangu pamoja na
Serikali katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukemea mauaji ya
vikongwe na albino. Sala zenu ndizo ambazo zimesababisha mimi
nikateuliwa na baba mtakatifu kuwa askofu na leo hii nimesimikwa rasmi
kuanza kazi katika jimbo hili la Shinyanga, nawaomba waumini wote
tushirikiane kwa pamoja katika kazi hii.”
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC),
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alimtaka Askofu Sangu kuchunga kondoo
wake aliokabidhiwa kwani wanahitaji upendo pamoja na kushirikiana vizuri
na wasaidizi wake katika kuleta maendeleo na kuwalea waumini kiimani.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Post a Comment