0
Morogoro. Watu 18 wameteketea kwa moto baada ya basi la Kampuni ya Nganga Express na lori aina ya Fuso kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Iyovi, Milima ya Uduzungwa, Morogoro
Katika ajali hiyo iliyotokea jana saa mbili asubuhi, abiria 15 waliokuwa kwenye basi na wengine watatu wa lori waliteketea kwa moto huku wengine 10 wakijeruhiwa vibaya.
Taarifa na picha za ajali hiyo zilianza kusambaa jana asubuhi kupitia mitandao ya kijamii zikionyesha masalia ya miili ya walioteketea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alisema ajali hiyo ilitokea baada basi hilo lililokuwa linatoka Kilombero kwenda Mbeya likiwa kwenye mistari ya barabarani ya katazo na kwenye mwendo kasi kugongana na lori lililokuwa limebeba matikiti na kuwaka moto.
Alisema majeruhi wanne wamelazwa katika Hospitali ya St. Kizito, Mikumi na sita wako katika Hospitali ya Mtandika, Iringa.
Alisema kwenye basi hilo kulikuwa na pikipiki ambayo pia iliungua na kusema inawezekana ndiyo iliyosababisha moto huo.
Ajali hiyo ni mfululizo wa ajali zinazotokea katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni siku moja baada ya watu watano kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mikoa ya Dodoma na Iringa saa 36, baada ya kumalizika mgomo wa madereva nchini.
AJALI MWAKA HUU
Aprili 9: Basi la Ngorika lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Arusha liligongana na basi la Ratco lililokuwa likitokea Tanga kwenda Dar es Salaam baada ya gari ndogo aina ya Toyota Passo iliyokuwa ikitokea Korogwe kuelekea Dar es Salaam kupoteza mwelekeo na kusababisha vifo vya watu 10.
Aprili 3: Ajali ya basi dogo la mashabiki wa klabu ya Simba SC Tawi la Mpira na Maendeleo (Simba Ukawa) eneo la Makunganya, Morogoro ilisababisha vifo vya watu saba na kujeruhi 24.
Machi 11: Watu 50 walifariki dunia na 22 kujeruhiwa katika ajali baada ya lori kugongana na basi la abiria la Kampuni ya Majinjah Express eneo la Mafinga Changarawe, mkoani Iringa.
Machi 22: Watu wawili walikufa na 22 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Itamboleo, wilayani Rujewa, Mbeya.
Februari 26: Watu watatu walifariki dunia papohapo baada ya lori la mafuta walilokuwa wamepanda kupinduka na kuwaka moto eneo la Wedi, katika Kijiji cha Maseyu mkoani Morogoro.
Januari 15: Watu wanne walifariki dunia baada ya basi la Hajees kupinduka katika Kijiji cha Mnazi, Kata ya Mandela wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Post a Comment

 
Top